Hofu familia ikiamkia vifaa vya ‘kishetani’
NA WANDERI KAMAU
HALI ya wasiwasi imekumba familia moja katika Kaunti ya Murang’a, baada ya kuamkia vifaa inavyovihusisha na uchawi, Jumamosi asubuhi, Januari 13, 2024.
Familia hiyo, kutoka kijiji cha Kahurura-Kirwara, eneobunge la Gatanga, ilipigwa na butwaa kwa kupata vifaa hivyo, ambavyo ilieleza haijui vilikotoka.
Vinajumuisha kifaa kinachofanana na jeneza, ndege anayefanana na mwewe, paka waliokuwa hai na wengine wameaga, kuku, njiwa kati ya vingine.
Baadhi ya viumbe hao walikuwa wamefungwa kwenye shingo zao na kengele.
Kwenye mahojiano, Bw Njenga wa Kahoya, alisema hajui vilikotoka vifaa hivyo vya kushtua.
“Hiki ni kioja na mshangao mkubwa kwa familia yangu. Hatujawahi kupata vifaa kama hivi. Tumeanza juhudi za kuyatakasa makazi yangu,” akasema Bw Njenga, aliyeongeza kuwa hana tofauti na mtu yeyote ama mvutano wote wa mali.
Kutokana na hofu kubwa iliyowakumba wakazi, walilazimika kumwita kaasisi wa Kanisa Katoliki ili kuyatakasa makazi hayo na kuwaepushia wanakijiji wengine dhidi ya kukumbwa na “mkosi” kama huo.
“Kando na kutakasa makazi ya Bw Njenga, lazima pia tujikinge dhidi ya kuandamwa na mkosi kama huu. Hivi ni vifaa vya kishetani. Ni vipi mtu anaweza kuvibeba na kuvileta hadi huku? Hizi ni nguvu za giza!” akasema Bw Muraguri Kimani, ambaye pia ni mkazi.
Kulingana na baadhi ya wazee, huenda kuna uwezekano familia hiyo ina mvutano wa mali, kama vile shamba na familia nyingine, au mtu fulani.
“Lazima kuna kiini cha tukio kama hilo. Katika jamii nyingi za Kiafrika, matukio kama hayo yalichangiwa na mvutano wa mali,” asema Mzee Githendu wa Karuri.