Habari Mseto

Hofu Kisauni ikidaiwa polisi wamegeuka majambazi

November 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

WAKAZI wa maeneo bunge ya Kisauni na Nyali kaunti ya Mombasa wanaendelea kuishi kwa hofu kufuatia kuzidi kwa mauaji ya kiholela yanayoendelezwa na magenge ya wahalifu.

Katika wiki moja pekee iliopita, watu watano wameuawa na wengine wengi kuachwa na majeraha baada ya mashambulizi yaliotekelezwa na magenge hayo.

Kisa cha hivi karibuni ni kile cha Jumapili usiku ambapo Samson Kinuthia mwenye miaka 42 alipigwa kwa panga hadi kufa katika eneo la Soweto.

Bw Kinuthia ambaye alikuwa muuzaji miraa eneo hilo alivamiwa na genge hili na kupigwa kwa panga kichwani.

Wakazi wa eneo hilo walisema kuwa wahusika walikuwa wahuni ambao wamekuja na mtindo mpya wa kujifanya maafisa wa polisi na kuibia watu.

Baadhi ya majeruhi waliongea na Taifa Leo walieleza kuwa iwapo hautakubaliana na wahuni hao basi hukupiga kwa panga hadi kufa.

“Tunaishi kwa hofu sasa. Mimi walinipiga na kuniumiza halafu wakachukua simu yangu pamoja na pesa nilizokuwa nazo. Hapa tulipofikia ni kuwa tunaogopa polisi na wahuni. Kila mmoja amekuwa mwoga,” akasema Bw Rajab Ali mmoja wa majeruhi.

Baada ya kumuua Bw Kinuthia ambaye ameacha watoto watatu, wahalifu hao walifululiza na kumpiga Bi Mercy Jilani na baadaye kumchoma kisu kwenye paja.

Mwathiriwa mwingine Bw Adam Kai aliingiliwa katika duka lake la Mpesa na watu hao waliokuwa wamevalia kama polisi.

“Baada ya kukataa kuwapatia pesa mmoja alitoa bunduki na baadaye wakanipiga kwa panga. Kitu nilichokumbuka saa chache baadaye ni kujikuta katika hospitali nikiuguza majeraha,” akasema Bw Kai huku akionyesha waandishi majeraha yake ya kichwa.

Visa hivyo vilitukia siku chache baada ya waendeshaji boda boda wawili kuuawa eneo la Mshomoroni siku ya Alhamisi na watu wengine wawili kukatwakatwa kwa panga mnamo Ijumaa usiku.

Matukio haya yamezua hisia baina ya wakazi pamoja na makundi ya kutetea haki za binadamu jijini humo.

Mashirika yakiwemo ya Commission for Human Rights and Justice (CHRJ), Muslims for Human Rights (Muhuri), Haki Yetu na Haki Africa yameyataka polisi kuchangamka na kuchunguza visa hivyo ambavyo vimeleta hofu.

Maafisa wa usalama kwa upande wao wamesema kuwa watachunguza visa hivyo kwa kina ili kutambua wahuni hao.