Hofu kwa familia mwanao kutoweka
RICHARD MAOSI NA MACHARIA MWANGI
FAMILIA moja katika kijiji cha Maiella, Naivasha inaishi kwa hofu baada ya mwana wao wa miaka 16, kupotea siku kumi zilizopita.
Mvulana huyo anayefahamika kama Peter Ngige,alikuwa shambani akipalilia shamba lao alipotoweka na tangu siku hiyo hajaonekana.
Naibu wa kamishna kitengo cha polisi, John Opondo alieleza wanahabari wa Nation kuwa huenda mvulana huyo alitekwa nyara akielekea nyumbani.
“Kabla simu yake haijazima alituma jumbe kadhaa akiwaonya ndugu zake na wazazi wasimpigie simu kwani alikuwa hatarini,” alisema bw Opondo.
Siku tano zilizopita jamaa zake waliokuwa wakimtafuta walieleza kuwa bw Opondo alipata baadhi ya mavazi yake yameroweka damu katika makazi ya kibinafsi.
“Vilevile walipata jembe na mapanga ambayo yanaaminika alitumia akiwa shambani,” alisema.
Ushirikiano baina ya familia majirani na maafisa wa polisi haujazaa matunda .
Bw Opondo alisema kuwa majasusi wapo katika harakati ya kutegua njama ya utekaji nyara.Vilevile alihimiza wakazi kutulia kwani mikakati imewekwa kumpata mvulana huyo.
“Tumewasilisha habari hizi kwa kiongozi wa idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai,ili atusaidie kutegua kitendawili hiki haraka,” aliongeza Opondo.