Hofu Mlima Kenya kwamba kutengwa kwa Gachagua kutaathiri kahawa, chai na maziwa
NA LUCAS BARASA
MADAI ya kutengwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika utawala wa Kenya Kwanza yameibua hofu Mlima Kenya haswa kuhusu hatma ya miradi yake kama vile kahawa, chai na maziwa.
Bw Gachagua pia amekuwa akihusika katika uendelezaji na utunzaji wa biashara ndogo ndogo, vita dhidi ya pombe haramu na mihadarati katika eneo hilo lililo na idadi kubwa ya wapigakura.
Naibu Rais ambaye amejiweka kama mtetezi mkubwa wa maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya kwenye serikali ya Kenya Kwanza hivi punde alianzisha mjadala mkali wa “mtu mmoja, kura moja, shilingi moja” ambao unashabikiwa na wengi eneo hilo kwa sababu unamaanisha kuongezewa mgao wa mapato.
Hofu ilijitokeza wazi Jumanne wakati wa ziara ya Bw Gachagua katika Kaunti ya Kirinyaga huku kila aliyezungumza akilalamikia matatizo katika sekta ya kahawa, chai kufuatia kucheleweshwa kwa malipo na vita dhidi ya pombe haramu ambavyo vimeonekana kukwama.
Kasisi wa kanisa la Kianglikana Kirinyaga Joseph Kibucwa alianzisha mjadala, akielezea wasiwasi wake kuhusu kucheleshwa kwa malipo ya kahawa kwa wakulima.
Alimwambia Naibu Rais katika Shule ya Msingi ya Ngungu wakati wa mazishi ya Mwalimu Mkuu wa zamani wa Shule ya Upili ya Kianyaga Kano Ndumbi kwamba wakulima walikuwa wanapoteza matumaini.
“Mimi ni mkulima wa kahawa na niliuza mazao yangu Desemba lakini kufikia sasa, sijapokea malipo yoyote,” alisema.
Kasisi Kibucwa alisema wakulima wengi walipanda kahawa nyingi wakiwa na matumaini makubwa kwamba watatajirika lakini sasa wamejawa na wasiwasi kufuatia kucheleweshwa kwa malipo.
“Mimi mwenyewe natumia mikopo kulipa wafanyakazi wanichumie kahawa na kunitunzia miti kwa sababu sijalipwa kwa mazao niliyouza Desemba. Sasa tunakaribia Juni na hatujapata chochote,” akalalama Kasisi.
Akijibu, Bw Gachagua alisema masuala yote ya malipo yalikuwa yanashughulikiwa.
Alisema serikali itafutilia mbali madeni ya wakulima kwenye vyama vya ushirika kama mojawapo ya njia ya kufufua sekta hiyo ya kahawa.
“Madeni yote yatafutwa ili wakulima waanze upya. Nimeongea na Rais na amekubali kwamba kama ilivyo kwamba madeni ya wakulima wa miwa yamefutwa, hivyo ndivyo itafanyika kwa wakulima wa kahawa. Waziri Simon Celugui (Wizara ya Vyama vya Ushirika) ameagizwa atayarishe hoja ambayo itapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kuidhinishwa ili tuanze upya,” alisema.