Habari Mseto

Hofu uzinduzi wa mtaala mpya wa 2-6-6-3 hapo 2019 utafeli tena

September 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

UZINDUZI wa mafunzo ya Mtaala mpya kwa madarasa ya chekechea hadi Darasa la Nne, Januari 2019, huenda ukagonga mwamba baada ya wachapishaji wa vitabu jana kulalama kuwa serikali haijatoa silabasi ya Darasa la Nne.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji (KPA) Lawrence Njagi alisema kuwa wanafunzi wa Darasa la Tatu ambao sasa wanafundishwa mtaala mpya huenda wakakosa vitabu watakapojiunga na Darasa la Nne mnamo Januari 2019.

Bw Njagi alisema kuwa wanafunzi walio katika Darasa la Tatu pia wako katika hatari ya kutumia mtalaa wa zamani wa 8.4.4.

Mtaala mpya wa 2-6-6-3 sasa unafanyiwa majaribio katika shule za chekechea hadi Darasa la Tatu na unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Januari mwaka ujao.

Mtaala mpya ambao unazingatia vipaji vya wanafunzi unatarajiwa kuchukua mahala pa mtaala wa zamani wa 8-4-4 kufikia 2027.

“Tumemwandikia barua waziri wa Elimu tukimtaka kutoa silabasi ya Darasa la Nne lakini hatujapata jibu. Hiyo inamaanisha kuwa vitabu vya darasa la Nne vitacheleweshwa kwani tumesalia na miezi mitatu pekee kumaliza mwaka,” akasema alipotangaza maonyesho ya Vitabu ya mwaka huu jijini Nairobi.

Afisa wa KICD, hata hivyo, aliwataka wachapishaji kuwa na subira huku akisema kuwa taasisi hiyo iko mbioni kuhakikisha kuwa vitabu vya Darasa la Nne vinachapishwa kabla ya kufunguliwa kwa shule katika muhula wa kwanza, mwaka ujao.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa wizara ya Elimu Kennedy Buhere alisema kwamba jukumu la kuandaa silabasi ni la KICD.

Chama cha KPA pia kilielezea wasiwasi wake kuwa kupunguzwa kwa bajeti ya Taasisi ya Uendelezaji wa Mitaala (KICD) huenda kukasababisha mpango wa kuzindua mtaala mpya kuanzia Januari mwaka ujao kutatizika.

Taasisi ya KICD ilikuwa imeomba Sh500 milioni kutoka kwa Hazina Kuu kwa ajili ya utekelezwaji wa mtalaa mpya lakini ikapewa Sh400 milioni.

“Elimu ya watoto ni muhimu kuliko barabara. Hivyo wizara ya Fedha haina budi kuongezea KICD fedha ili kuhakikisha kuwa mtaala mpya unatekelezwa bila kuwepo vikwazo vya pesa,” akasema.

Wakati huo huo, Chama cha KPA kiliwaondolea wazazi wasiwasi huku kikisema kuwa bei ya vitabu haitaongezwa kutokana na kuletwa kwa Ushuru wa Thamani ya Ziada wa asilimia 8 unaotozwa mafuta.

Bw Njagi alisema bei ya vitabu inadhibitiwa na serikali na hivyo basi wachapishaji hawana uwezo wa kupandisha bei bila kupata idhini.

Lakini tukilemewa na ushuru tutaandikia wizara ya Fedha barua tukiitaka kuturuhusu kupandisha bei ya vitabu,” akasema Bw Njagi.

Maonyesho ya vitabu ambayo hufanyika kila mwaka yatang’oa nanga Septemba 26 na kumalizika Septemba 30.

Maonyesho hayo yatafunguliwa rasmi na kinara wa ODM Raila Odinga Septemba 27.

“Bw Odinga alipewa hadhi ya kufungua maonyesho hayo kwa sababu ni kiongozi mtajika na vilevile mwandishi wa vitabu,” akasema mwandalizi wa maonyesho hayo Bi Mary Maina.