Hofu Ziwa Victoria likinyakuliwa na wafanyabiashara
NA GEORGE ODIWUOR
HOFU imezuka kuhusu hatima ya wavuvi katika Ziwa Victoria, baada ya kubainika kampuni za kibinafsi zimetwaa sehemu kubwa za ziwa hilo kufanyia ufugaji wa samaki.
Wavuvi ambao tayari wanakumbwa na matatizo ya uchafuzi wa ziwa uliopunguza idadi ya samaki, pamoja na ushindani kutoka kwa wafanyabiashara wa samaki wa bei ya chini wanaotolewa Uchina, sasa wanaelekea kukumbwa na taabu zaidi kwani hawaruhusiwi kufanya uvuvi karibu na sehemu zinazotumiwa na kampuni hizo ziwani.
Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ jana alilalamikia vikali jinsi wavuvi wenyeji wananyimwa nafasi ya kujitafutia riziki.
Kulingana naye, hekta 315 za Ziwa Victoria katika eneobunge la Suba Kusini pekee zimetwaliwa na wawekezaji wa kibinafsi wanaofuga samaki.
Alisema nafasi nyingine zilizotwaliwa ziwani ni ekari 23 katika ufuo wa Gingo na hekta 212 katika kaunti jirani za Migori, Siaya na Kisumu.
“Sipingi ufugaji wa samaki ndani ya ziwa, lakini kasi ambayo inatumiwa na wawekezaji wa kampuni mbalimbali kutwaa sehemu ya Ziwa Victoria kwa shughuli za uvuvi inatisha na inafaa kudhibitiwa.
“Tunafahamu kwamba wawekezaji wanafaa kutumia ardhi nje ya ziwa kuchimba vidimbwi na kuwafuga samaki, lakini sasa wamehamia ziwani na kuna hatari kwamba Ziwa Victoria huenda likatwaliwa na wawekezaji wa kibinafsi,” akasema Bw Kajwang’.
Mfanyabiashara maarufu katika eneo hilo, Bw Jima Akali alitaja tabia ya wawekezaji hao kama chanzo kikuu cha wavuvi kukosana na maafisa wa usalama katika mataifa jirani ya Uganda na Tanzania.
Vilevile, wavuvi katika eneo la Sindo walikashifu mienendo hiyo ya kampuni za kibinafsi huku wakihofia huenda wakashindwa kujikimu kimaisha hivi karibuni, kwani sehemu nyingine za ziwa zimejaa magugu na uvuvi hauwezi kufanywa huko.
Wakiongozwa na Bw Okambo Kisiara, wavuvi hao walitoa mfano wa kampuni moja, ambayo walisema husogesha nafasi zaidi hadi ndani ya ziwa nyakati za usiku, na kuwakosesha wavuvi maeneo ya kushiriki uvuvi, mbali na kuwa mbinu mbovu hutumiwa katika ufugaji huo na kuhatarisha uwepo wa samaki wengine ziwani.
“Hizi kampuni hufuga aina ya samaki ambayo ni hatari kwa samaki wengine na hivyo kuhatarisha mapato ya wavuvi. Baadhi ya lishe wanazotumia ziwani pia hazijaidhinishwa na zinaweza kumaliza kizazi chote cha samaki,” akasema Bw Kisiara.