• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
HOMA BAY: Naibu Gavana ashika usukani Awiti akitibiwa

HOMA BAY: Naibu Gavana ashika usukani Awiti akitibiwa

NA CECIL ODONGO

GAVANA wa Homa Bay Cyprian Awiti amemwachia Naibu wake Hamilton Orata majukumu ya kuendesha kaunti hadi atakapopata afueni baada ya kufanyiwa upasuaji wa macho majuma kadhaa yaliyopita.

Kulingana na msemaji wake, Juma Aluoch, Bw Awiti hata hivyo ataendelea kuhusika na masuala ya kaunti hiyo na wakazi wa Homa Bay hawafai kuwa na hofu kuhusu utoaji wa huduma.

“Masuala ya kaunti yataendelea kuendeshwa na Naibu Gavana jinsi ambavyo amekuwa akifanya wakati gavana alikuwa akipokea matibabu. Hakuna haja ya taharuki kwa sababu huduma bado zitatolewa kama kawaida,” Bw Aluoch aliambia Taifa Leo jana.

Bw Awiti hajaonekana hadharani kwa miezi kadhaa, hali ambayo imeibua wasiwasi miongoni mwa wakazi huku baadhi ya viongozi wa kisiasa wa kaunti hiyo wakimtaka ajiuzulu wadhifa wake na kupisha uongozi mpya.

Seneta Moses Kajwang na Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma wameibua masuala kadhaa kuhusu jinsi masuala ya kaunti yamekuwa yakiendeshwa, wakilalamikia kukithiri kwa visa vya ufisadi kwenye serikali ya gavana huyo.

“Gavana anafaa kujiuzulu kwa kuruhusu mawaziri wake kushiriki ufisadi bila kuchukuliwa hatua. Serikali yake haijatoa huduma zozote za maendeleo na ni kama kwamba shughuli zote za kaunti zimesitishwa. Hatua za dharura zinahitajika kuokoa kaunti hii,” akasema Bw Kaluma kwenye mahojiano na Taifa Leo.

“Tunataka uongozi wa kaunti utwaliwe na serikali kuu kisha uchaguzi uandaliwe baada ya siku 90 kumteua gavana mpya. Binafsi, sina nia ya kuwania kiti cha ugavana 2022 lakini najuta sana kumpigia debe Bw Awiti mnamo 2017,” akaongeza Bw Kaluma.

Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang wiki chache zilizopita pia alidai kwamba, uongozi wa kaunti hauna nafasi kwa wataalamu na akasisitiza hakuna mabadiliko ambayo yameonekana kwenye uongozi wa Bw Orata ambaye amekuwa akitekeleza majukumu kwa niaba ya gavana kwa miezi kadhaa sasa.

Hata hivyo, Bw Aluoch aliwashtumu viongozi hao wawili kwa kuipaka tope serikali ya kaunti wakilenga siasa za 2022.

“Gavana Anyang Nyong’o wa Kisumu na John Nyangarama wa Nyamira waliwahi kuugua na masuala ya kaunti yao yakaendeshwa na manaibu wao lakini hakuna malalamishi yaliyotokea kama tunayoyashuhudia hapa Homa Bay. Viongozi hawa wanafaa kumpa gavana nafasi ya kutumikia raia,” akaongeza Bw Aluoch.

Kauli ya Mabw Kajwanga na Kaluma iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bunge la Wenye Nchi, Kaunti ya Homa Bay Walter Opiyo ambaye aliapa kutumia shughuli aliyoanzisha ya kukusanya saini kumwondoa gavana huyo ofisini.

“Haya mambo yanayotokea sasa niliyaona zamani. Wananchi wa kaunti hii wanajuta sana na wengi walitarajia kungekuwa na uchaguzi mdogo kutokana na kesi iliyowasilishwa mahakamani na Bw Oyugi Magwanga

“Mchakato wa kukusanya saini haujasambaratika kamwe. Tayari, tumekusanya saini 50,000 na kufikia mwisho wa mwaka huu nitakuwa nimekusanya vitabu vyote na kutimiza idadi inayohitajika kisheria kisha nimkabidhi Rais Uhuru Kenyatta ili aivunjilie mbali kaunti hii,” akasema Bw Opiyo.

You can share this post!

Taharuki KDF kuua watu 3 kwa risasi kabla ya kujiangamiza

Diwani ailaani serikali ya kaunti kuwanyima walemavu ajira

adminleo