Hospitali mpya ya rufaa ya KU yapokea wagonjwa wachache siku ya kwanza
Na LAWRENCE ONGARO
LICHA ya hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kufunguliwa rasmi Jumatatu, bado wagonjwa hawajafurika jinsi ilivyotarajiwa.
Ijumaa wiki jana, Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki na wakuu wa bodi ya hospitali hiyo walitangaza kuwa Rais Uhuru Kenyatta angefungua hospitali hiyo Jumatatu kukiwa na matumaini wagonjwa wangekuwa wengi.
Uchunguzi uliofanywa umebainisha kuwa ni wagonjwa wawili tu ndio walifika mnamo siku ya kwanza ya huduma katika hospitali hiyo.
Mzazi kwa jina Bw Kennedy Mweru, alimpeleka mwanawe ili achunguzwe maradhi ya kifafa ambayo yamemsumbua mwanawe kwa muda mrefu.
“Hapo awali nilikuwa nimempeleka mtoto katika hospitali binafsi, lakini baadaye nikapewa mwongozo niende katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH). Kwa upande mwingin, nilihiari nimlete mtoto wangu katika hospitali mpya ya rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ili atibiwe,” alisema Bw Mweru.
Hata hivyo, ikizingatiwa ilikuwa ni mara ya kwanza kwa hospitali hiyo kufunguliwa, matarajio ni kwamba itazidi kupata wagonjwa baada ya siku chache zijazo.
Kulingana na Bi Kariuki alipozuru hospitali hiyo wiki jana, alisema ya kwamba ujenzi wa hospitali hiyo uligharimu takribani Sh8.8 bilioni ambapo aliisifia kiasi cha kulinganishwa na zile za kimataifa.
Idadi ya madaktari na wauguzi
Mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo Profesa Olive Mugenda alisema itakaposhika kasi katika shughuli zake, wagonjwa wengi watapata matibabu ya hali ya juu kwa sababu tayari wametuma madaktari waliyohitimu 40 na wauguzi kadha.
Daktari mkuu na msimamizi wa hospitali hiyo Dkt Andrew Toro alikuwa ameelezea hapo awali kuwa hospitali hiyo itakuwa ikitibu na kushughulikia maradhi sugu kama ya saratani na yaliyo na historia ndefu, wale sio maradhi madogomadogo kama homa na kichwa kuwanga.
Hospitali hiyo imejengwa kupitia juhudi zake Prof Olive Mugenda wakati alikuwa Naibu Chansela wa KU miaka michache iliyopita.
Miezi michache iliyopita hospitali hiyo ilikuwa imetangaza nafasi za kazi katika sekta tofauti ambapo tayari nafasi nyingi zimejazwa ili kazi za hospitali hiyo zianze rasmi.