Habari Mseto

Hospitali ya Igegania Gatundu kupata sura mpya

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI ya Igegania eneo la Gatundu Kaskazini itafanyiwa ukarabati ili iweze kuhudumia wakazi wa Mang’u na vitongoji vyake.

Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro alisema kwa muda mrefu hospitali hiyo imekuwa katika hali mbaya bila kurekebishwa.

“Kaunti ya Kiambu itafanya marekebisho mkubwa kwenye hospitali hiyo ili wakazi wa Mang’u na maeneo yaliyo karibu wapate huduma ya karibu,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema vifaa muhimu vitawekwa ambapo maabara ya kisasa pia itajengwa.

Chumba cha kujifungulia wanawake wajawazito, na jikoni zitajengwa pia.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba mitambo ya kisasa ya kufulia nguo inawekwa katika hospitali hiyo. Hata tunatarajia kupandisha cheo hospitali hiyo kuwa katika kiwango cha Level 5,” alisema gavana huyo.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jana alipozuru hospitali hiyo ili kujionea jinsi inavyofanyiwa marekebisho.

Alisema hospitali zote za Kiambu ziko na dawa ambapo hakuna mgonjwa anayestahili kulalamika kuhusu ukosefu wa dawa hospitalini.

“Kulingana na wakazi wengi tayari wameridhika na mpango huo ambapo dawa zinapatikana hospitalini bila shida,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema hospitali ya Gatundu Level 5 itapandishwa cheo iwe kiwango cha Level 6.

Alisema kwa sasa hospitali ya Tigoni Level 4 ina vitanda 230 vya wagonjwa wa Covid -19.

Wakati huo pia Wizara ya Afya imehifadhi hewa ya oksijeni kwenye mtungi mkubwa ambapo wagonjwa mahututi wa Covid-19 wanapokea matibabu bila shida.

Alisema Kaunti ya Kiambu itaangazia zaidi maslahi ya madaktari na wauguzi ili waweze kutekeleza wajibu wao kwa njia inavyostahili.

“Tayari tumechukua mwelekeo mpya wa kupambana na Covid-19 ambapo Wizara ya Afya inafanya juhudi kuona ya kwamba wagonjwa wanashughulikiwa jinsi inavyostahili,” alisema Dkt Nyoro.