Habari Mseto

Huduma katika kivuko cha Mtongwe zarejelewa

September 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DIANA MUTHEU

WAKAZI wanaotumia kivuko cha feri cha Mtongwe, katika kaunti ya Mombasa walijawa na furaha baada ya huduma kurejea leo asubuhi.

 Huduma za feri katika kivuko hizo zilikuwa zimesitishwa kwa muda wa mwaka mmoja sasa, huku shirika la Huduma za Feri Nchini (KFS) ikisema kuwa ilikuwa inataka kukarabati kivuko hicho.

Feri ya MV Kwale ilitumika kuwasafirisha wakazi kutoka upande mmoja hadi mwingine.

Wakizungumza na Taifa Leo, wakazi hao wameiomba serikali kuhakikisha kuwa feri hiyo haiondolewi tena katika kivuko hicho.

“Tumekosa huduma ya feri hii kwa kipindi cha mwaka mmoja sana. Pia, hapo awali, feri ilikuwa inaletwa katika kivuko hiki, kisha miezi chach baadaye inaondolowa na wakazi wanabaki wakihangaika. Tungeomba tuhakikishiwe kuwa shughuli katika kivuko hiki zitaendelea bila kusimamishwa,” akasema Bw John Wenje ambaye ni mkazi wa Mtongwe.

Bw Wenje aliomba viongozi wasitumie tena kivuko hicho wanapoendeleza siasa zao.

“Feri hii iletwe kuwasaidia wakazi wa Mtongwe na tunaomba siasa ziwekwe kando kabisa,” aksema.

Abiria wakishuka kutoka kwa feri katika kivuko cha Mtongwe. PICHA/ DIANA MUTHEU

Mkazi wingine, Stephen Kasyoki alisema kuwa kusitishwa kwa huduma katika kivuko hicho kuliwalazimisha kutumia kivuko cha Likoni kinachoshuhudia msongamano mkubwa watu na magari.

Bw Kasyoki alisema kuwa walilazimika kulipa Sh30 au zaidi kutoka eneo la Mtongwe hadi kivuko cha Likoni, na Sh30 hadi jijini Mombasa.

“Kwa siku tulilazimika kutumia hadi Sh200 kwa nauli, lakini kwa kuwa huduma za feri katika kivuko cha Mtongwe zimereje, hatutumii nauli yeyote,” akasema Bw Kasyoki.

Mwenyekiti wa chama cha watumizi wa kivuko cha feri ya Mtongwe, Bw Michael Ogwambo alisema kuwa itakuwa afueni kwa watumizi wa kivuko hicho ikiwa watawekewa sabuni na mifereji ya maji safi, ili waweze kujikinga na virusi vya corona.

“Tumewahimiza wasafiri wote wavalie barakao zao kabla ya kuabiri feri na pia waketi au kusimama kwa umbali wa mita moja unusu,” akasema Bw Ogwambo.

Bw Ogwambo anasema kuwa baadhi ya marekebisho ambayo wameshuhudia ni kama mbao mpya kuwekwa katika jeti, na vyuma vipya kuwekwa wanaposhukia na kuabiria feri hiyo.