HUDUMA NAMBA: Chifu aamriwa awalipe makurutu wa ziada Sh40,000
Na MWANGI MUIRURI
Jopo maalumu la kiusalama katika Kaunti ya Murang’a limemwamrisha chifu mmoja eneo hilo awalipe makurutu watano aliokuwa amewasajili kushiriki warsha ya mradi wa Huduma Namba lakini wakakosa kuajiriwa kazi.
Bw Muiruri Kabugua aliamrishwa akiwa chifu wa wadi ya Kahumbu kulipa jumla ya Sh40, 000 ambazo zilikuwa marupurupu ya makurutu waliokuwa wameshiriki warsha hiyo ya siku tano katika ukumbi wa Kigumo na ambapo kila mmoja alikuwa akipokezwa Sh10, 000.
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Kigumo, Bi Margaret Nyambura, chifu huyo alipatikana na makosa ya kukiuka maelezo ya usajili ikama yalivyokuwa yametolewa na wizara ya usalama wa ndani.
“Ikiwa wadi yake ilikuwa imepewa nafasi nne kwa kila wadi, hakuwa na kisingizio chochote cha kusajili idadi ya juu. Nilifumbua kulikuwa na shida wakati wa kutoa malipo hayo na ndipo kulizuka mtafaruku ambapo msemaji Wa waathiriwa hao, Anne Wairimu Ngigi aliongoza harakati za kudai pesa zao,” akasema.
Bi Nyambura anasema kuwa baada ya kupekua orodha yake ya makurutu aligundua kuwa kulikuwa na idadi ya juu ya waliosajiliwa na licha ya kushirikishwa uhamasisho wote na kisha kulisha kiapo cha huduma, hawakupewa kazi na hawakulipwa marupurupu yao.
“Ndipo tuliandaa jopo spesheli la uchunguzi na matokeo yakawa ni amri kuwa chifu huyu awalipe makurutu wake wote ambao alisajili kinyume na sheria. Na ameamrishwa kufanya hivyo mara moja la sivyo aadhibiwe kwa kuwa serikali haiwezi kuwa ya kufanya kazi kwa mzaha na hadaa kwa hata watoto wanaotafuta kazi,” akasema.
Kamishna wa Kaunti hiyo, Mohammed Barre alisema kuwa ameamrisha uchunguzi utekelezwe kubaini kama kuna dosari katika orodha ya waliopewa kazi na idadi inayohitajika katika mradi huo.
“Kuna uwezekano kuwa kulikuwa na njama ya kupunguza wale waliopewa kazi ili pesa zao baada ya harakati hizi zitwaliwe na baadhi ya matapeli katika huduma ya serikali. Hilo halitawezekana nikiwa Kamishna hapa na onyo langu ni kuwa, afisa yeyote ambaye anajua ni mfisadi anafaa kujitoa mapema kutoka huduma ya serikali hapa Murang’a
kwa kuwa nitamhangaisha hadi kushtakiwa,” akasema.
Harakati za makarani hao wa kushirikisha usajili wa Wakenya kwa mfumo wa huduma namba zilitamatika Jumamosi iliyopita.