• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Huduma Namba si ile ‘666’ ya kishetani, Uhuru awaambia Wakenya

Huduma Namba si ile ‘666’ ya kishetani, Uhuru awaambia Wakenya

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne aliwakemea wanaodai kwamba shughuli ya kusajili Wakenya kwa njia ya kielektroniki, maarufu kama Huduma Namba, ni ya kishetani.

Rais aliwaambia viongozi wa kidini wakome kuwapotosha Wakenya kwa kuhusisha shughuli hiyo na ushetani.

“Wacheni kupotosha Wakenya kwa kueneza uongo kuhusu shughuli hii. Nimesikia eti ni ya kishetani,” alisema Rais Kenyatta.

Baadhi ya viongozi wa makanisa wamedai kwamba Huduma Namba ni sawa na nambari 666 iliyotabiriwa katika Bibilia, madai ambayo Rais Kenyatta alikanusha jana.

“Mimi kama Mkristo ninashangaa ninaposikia baadhi ya mapasta wakisema hii ni ishara ya kishetani. Je, shetani na kujitambulisha wana uhusiano gani,” aliuliza Rais Kenyatta.

Alitaja madai ya wahubiri hao kama upuuzi mtupu, na kuwataka wakome kuwapotosha Wakenya kuhusu shughuli hiyo.

Rais alisema lengo la usajili huo ni kuimarisha uwezo wa Wakenya kupata huduma wanazohitaji.

Rais pia alikanusha kwamba Wakenya watatolewa damu kupimwa DNA kwenye shughuli hiyo ili habari hizo zihusishwe kwenye Huduma Namba.

“Nimesikia upuzi mwingine kwamba wanaume walio na mipango ya kando na wamezaa watoto nje watajulikana kwenye usajili huu baada ya kupimwa DNA. Hizi ni propaganda,” akasema.

Kuhusu hofu ya usalama wa habari za watu binafsi zitakazokusanywa kwenye shughuli hiyo, Rais Kenyatta alisema serikali inaandaa sheria ambayo itathibiti upatikanaji wa habari kuhusu mtu binafsi.

“Tuko mbioni kuandaa sheria ambayo itathibiti usambazaji wa habari na kuhakikisha kwamba habari hizo zitalindwa,” akaeleza.

Mnamo Jumatatu, mahakama ilizuia serikali kujumuisha rekodi za chembechembe za damu maarufu kama DNA kwenye usajili huo. Pia iliagiza serikali kutotoa habari zitakazokusanywa kwa shirika au mataifa mengine.

You can share this post!

TAHARIRI: Kaunti zilizozembea kuwafaa wananchi zichunguzwe

ODM yasukuma Uhuru awapige kalamu mawaziri ‘fisadi’

adminleo