Habari Mseto

Huenda serikali ikakwama, wabunge waambiwa

February 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LYNET IGADWAH na CHARLES WASONGA

MZOZO umeibuka kati ya ofisi mbili za Serikali zinazohusika na masuala ya pesa, kuhusu bajeti ya mwaka ujao wa kifedha.

Hii ni baada ya ofisi ya Msimamizi wa Bajeti (CoB) kuibua shauku kuhusu uwezo wa Kenya kumudu mahitaji yake ya kifedha.

Hii ni kufuatia hali kuwa taifa litatumia asilimia 61 ya mapato yake katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 kulipa madeni.

Katika Mwongozo wa Bajeti ya 2019 inayochanganuliwa bungeni wakati huu, Hazina Kuu inapendekeza kuwa katika ya Sh1.87 trilioni zinazotarajiwa kukusanywa mwaka huu, Sh1.1 trilioni zitumike kulipia madeni ya serikali.

Kulingana na viwango vya kimataifa, uchumi wa nchi unakuwa hatarini ikiwa mzigo wa madeni utatimu asilimia 70 ya utajiri wa nchi.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha wa Fedha Henry Rotich anashikilia kuwa deni la sasa la takriban Sh5.3 trilioni sio hatari kwa uthabiti wa uchumi.

“Ikiwa Sh1.1 trilioni zitaelekezwa kulipia madeni, hii ina maana kuwa zitasalia Sh700 bilioni pekee ya matumizi. Hizi haziwezi kutosha kufadhili mahitaji ya uchumi. Bunge la linapasa kushauri Hazina Kuu kuangalia upya sera zake za kifedha ili kuzuia kukwama kwa shughuli za serikali,” Bw Joshua Musimu, ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango katika afisi ya Bajeti, aliambia Kamati ya Seneti kuhusu Fedha jana.

“Tunahisi kuwa kiwango cha madeni kielekea hivi uchumi wa nchi utakuwa hatarini. Lakini kila tunapoonya Hazina Kuu kuhusu hatari ya mzigo huu wa madeni, wao hutupatia hakikisho kwamba tuko salama,” akasema Bw Musyimi, akiongeza kuwa madeni hayo yamekuwa yakizaa riba ya juu kupindukia.