Habari Mseto

Huenda shule zifunguliwe Oktoba 19

September 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na FAITH NYAMAI

SHULE huenda zikafunguliwa Oktoba 19, iwapo serikali itakubali mapendekezo ya kamati inayosimamia masuala ya elimu nchini katika kipindi hiki cha kukabili virusi vya ugonjwa wa Covid-19.

Kulingana na ripoti ya kamati hiyo, wanafunzi wa Darasa la Nane na wale wa Kidato cha Nne watafanya mitihani yao ya kitaifa ya KCPE na KCSE mtawalia mwezi wa Aprili mwaka ujao.

Kamati hiyo imependekeza pia kalenda ya shule za msingi na upili kubadilishwa ili muhula wa kwanza uwe ukianza Juni.Hapo kesho, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, anatarajiwa kuipokea ripoti hiyo ya kamati.

Inatarajiwa baadaye wadau watashauriana na Rais Uhuru Kenyatta ambaye ataidhinisha uamuzi wa mwisho utakaotolewa.

Kwenye mapendekezo yake ya kwanza, kamati hiyo inataka wanafunzi wa Darasa la Saba na Nane, Kidato cha tatu na cha Nne warudi shuleni Jumatatu, Oktoba 19.Wanafunzi wa Darasa la Nne, ambao ndio wa kwanza kutumia mtaala mpya wa masomo, wanatarajiwa kuripoti shuleni siku hiyo pia.

Wanafunzi wengine wote watarejea shuleni baada ya wiki mbili.“Mapendekezo haya ni ya kuzipa nafasi shule kujitayarisha kuwapokea wanafunzi kwa zamu,” duru zilisema.

Kwenye mapendekezo ya pili, kamati hiyo imependekeza wanafunzi wote kuripoti shuleni siku moja, Oktoba 19.

Prof Magoha anatarajiwa kuwasilisha ripoti hiyo wakati wa mkutano wa kitaifa kuhusu janga la corona, mnamo Septemba 25.

Mkutano huo utaongozwa na Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i na Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe.Ijumaa, Prof Magoha aliwaambia waalimu waanze kujipanga kurudi shuleni lakini akadinda kusema shule zitafunguliwa lini.

“Ugonjwa huu umeanza kupungua nchini, walimu wanafaa kuanza kujitayarisha kurudi shuleni. Tutawapa wanafunzi wanaongojea mtihani fursa ya kwanza kurudi shuleni,” alisema Prof Magoha.

Wakati alipozuru karakana za kutengeneza madawati ya shule Nairobi, Rais Kenyatta alisema serikali iko tayari kusaidia shule kufunguliwa.

Serikali imetenga Sh1.9 bilioni kutengeneza madawati ya shule za msingi na zile za sekondari.Prof Magoha aliwaelekeza wakurugenzi wa elimu wa maeneo na kaunti kuhakikisha madawati hayo yamefika shuleni ifikapo Oktoba 19.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (Kesha), Bw Kahi Indimuli alisema wako tayari kufungua na kuwaomba wadau wengine kujitokeza na kusaidia shule kujiandaa.

Bw Indimuli alisema kwa sasa, wadau tofauti wamejitokeza kusaidia shule za sekondari na vifaa vya kupima joto la mwili shuleni.“Tunawaomba wengine ambao wana uwezo wa kununua barakoa, sabuni na matangi ya maji wajitokeze,” akasema.

Mkuu wa chama cha walimu wakuu wa shule za msingi (Kepsha), Bw Nicholas Gathemia alisema kuwa walimu wakuu wanasubiri maagizo kutoka kwa wizara ya elimu.

“Kwa sasa matayarisho machache yamefanywa kwenye shule za msingi lakini tuna hakika serikali itatupa msaada unaofaa katika wiki zijazo,” alieleza Bw Gathemia.

Katibu mkuu wa muungano wa waalimu za sekondari (Kuppet), Bw Akelo Misori pia alisema wakati umefika wa shule kujiandaa kufunguliwa.