Huwezi kuua mwanamke kwa madai ya kurekebisha tabia – Kate Actress
NA FRIDAH OKACHI
MWIGIZAJI Catherine Kamau almaarufu Kate Actress alijongea maandamano ya amani mjini Nyeri Ijumaa wakati wa kusilisha ombi kwa Kamshna wa Kaunti ya Nyeri, Pius Murugu, kutokana na mauaji ya kiholela ya wanawake nchini Kenya.
Katika ujumbe aliochapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa miaka 36, alisema Kamshna wa Kaunti hiyo amewahakikishia kumaliza mauaji hayo na kuendelea kusaidia waathiriwa.
Wakati wa maandamano hayo, mwigizaji huyo alilaani vitendo vya mauaji dhidi ya wanawake, akisema kuwa wanawake wana haki ya kuishi.
“Mimi ni mama, nina binti, tuna haki ya kuishi. Dada zangu wana haki ya kuishi. Nina jukumu la kulinda na kuzungumzia kuhusu mauaji yoyote au dhuluma yoyote ambayo ni kinyume na haki ya kuishi,” alisema Kate Actress.
Mama huyo wa watoto wawili alidai kuwa mauaji yanayotekelezwa kwa wanawake hayafanyiki katika vyumba vya kukodi tu, ila idadi ya juu ya mauaji hayo yanatekelezwa nyumbani na watu wanaofahamu wanawake hao.
“Mwaka 2016 hadi sasa mauaji ya wanawake nchini ni 542. Mauaji 245 yanahusishwa na wanaume nyumbani. Hii kitu mnasema eti ni vyumba vya kukodi, sio sababu kuu. Wanawake 245 wameuliwa na wanaume wao nyumbani kwao. Hii sio kuhusu tuu maadili bali ni kibinadamu. Wanawake wana haki ya kuishi, na tunafanya maandamano haya kutaka vifo hivi kusitishwa. Wanawake wanauliwa na watu wanaowafahamu na sio wageni kwao,” alisisitiza Kate Actress.
Kati ya idadi hiyo, ni 99 wameuliwa na watu wasiojulikana. Ripoti ya mauaji kutoka Umoja wa Mataifa chini ya kitengo cha Dawa na Uhalifu, inaonyesha kuwa mwaka wa 2023, ulirekodi idadi ya juu ya mauaji ya wanawake na kufikia 150.
Wiki jana Grace Wangari Thuiya, 24, alisaidiwa na maafisa wa polisi katika mtaa wa Githurai, waliokuwa wakipiga doria na kusikia vurugu nyumbani kwake.
Walimuokoa mama huyo wa mtoto mmoja ambaye alikuwa amechomwa visu mara kadhaa na kupelekwa katika hospitali ya Kiambu Level 5 akiwa hali mahututi na kupoteza maisha yake.