Habari MsetoSiasa

Huyu ndiye kiongozi anayenuia kumrithi Prof Kivutha Kibwana

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Pius Maundu

NAIBU Gavana wa Makueni Adelina Mwau ametangaza kuwa ana azma ya kugombea ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Gavana Kivutha Kibwana atakapostaafu.

Hatua yake inafikisha wanaopanga kuwania kiti hicho kufika wawili.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior tayari ametangaza kuwa atagombea ugavana 2022. Bi Mwau alisema ndiye anayefaa kumrithi Profesa Kibwana kwa sababu wamekuwa wakishirikiana vyema tangu walipochaguliwa 2013.

“Nitarudi hapa kuomba kura za ugavana kwa sababu ninatosha kulinda sifa za Makueni,” alisema Jumamosi akiwa kijiji cha Kee wakati wa karamu ya kustaafu kwa Bi Benedette Muema, aliyekuwa mwalimuwa shule ya msingi ya Kasunguni.

Ilikuwa mara ya kwanza ya Bi Mwau ambaye pia alikuwa mwalimu, kutangaza kuwa anamezea mate kiti cha ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Mnamo Juni mwaka huu alikasirisha baadhi ya watu alipodai kuwa kiti cha Profesa Kibwana hakifai kukaliwa na watu wasioweza kulinda kazi nzuri ambayo ametekeleza. Gavana Kibwana amekuwa akiwataka viongozi kuzingatia maendeleo badala ya siasa za 2022.