Habari Mseto

Huzuni 4 wakifariki kwenye ajali nyingine Meru

April 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

WATU wanne walithibitishwa kufariki Jumapili, Aprili 7, 2024, baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuanguka katika daraja la Nithi, kwenye barabara kuu ya Meru-Nairobi.

Mkurugenzi wa Huduma za Uokoaji katika Kaunti ya Meru, Bw Alex Mugambi, alisema kuwa watu kadhaa walikimbizwa katika hospitali kadhaa katika kaunti hiyo.

Basi hilo, ambalo lilikuwa likisafiri kutoka eneo la Maua, Meru, lilikuwa na abiria 39 lilipopata ajali hiyo.

Aidha, linamiliwa na kampuni ya Kensilver.

Ripoti zilieleza kuwa lilianguka baada ya kupata matatizo ya breki.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Tharaka –Nithi, Bw Zacchaeus Ng’eno, alithibitisha ajali hiyo, akisema kuwa abiria wanne walithibitishwa kufariki huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Bw Ng’eno alisema kuwa kiini cha ajali hiyo bado hakijajulikana.

Hata hivyo, alisema kuwa polisi wameanza uchunguzi kubaini kiini cha ajali hiyo.

“Bado tunaendeleza uchunguzi kubaini kiini cha ajali hiyo. Ripoti tulizo nazo ni kwamba watu kadhaa wamefariki,” akasema Bw Ng’eno.

Bw Ng’eno alirai madereva kuwa waangalifu wakiwa barabarani na kuhakikisha magari yako katika hali nzuri ili kuepuka ajali zaidi.

Hilo linajiri huku Wakenya wengi wakiendelea kulalamikia ongezeko la ajali zaidi nchini.