Huzuni polisi akiangamiza wanawe wawili, shemeji na kujitoa uhai
POLISI katika kaunti ya Homa Bay wanachunguza kisa ambapo afisa mmoja wa polisi aliwaua wanawe wawili na shemejiye kabla ya kujitoa uhai.
David Okebe Goga, anayehudumu katika Kaunti ya Marsabit, aliwaua watoto wake Triza Okebe, Hazad Okebe na shemeji yake Seth Odeka, wote wenye umri wa kati ya miaka mitano na saba.
Wapelelezi wanasema aliwaua kwa kuwawekea sumu katika chakula.
Aidha, inaripotiwa kuwa alitisha kumuua mmoja wa wakubwa wake, aliyemkasirisha, lakini baadaye akabadilisha nia.
Okebe, ambaye ni afisa wa cheo cha Konstebo, aliandika maelezo haya yote kwenye taarifa iliyopatikana Jumapili, Aprili 6, 2025 pamoja na maiti yake nyumbani kwake kijiji cha Kagoga, kata ya Kakdhimu Mashariki, Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Kaskazini.
Watu wengi katika kijiji hicho walidhani kuwa marehemu alikuwa amerejea nyumbani, wiki tatu zilizopita, kwa mapumziko ya kawaida.
Lakini Okebe alikuwa na lengo lingine.
Kulingana na polisi, ilionekana kuwa alirejea nyumbani kwa lengo la kujiua na kuua wanawe wawili na shemejiye.
Miili ya wanawake, Triza na Hazad, ilipatikana katika kitanda kimoja, ndani ya chumba cha kulala huku mwili wa Seth ukipatikana katika chumba cha kupokea wageni.
Maafisa wa upelelezi waliambia Taifa Dijitali kwamba pofu ilikuwa ikitoka midomoni mwa watoto hao ishara kwamba walipewa sumu.
Chupa za soda na vipande vya mkate ambavyo wapelelezi waliamini vilitiwa sumu, pia vilipatikana eneo la mkasa.
Bw Fred Ochieng, ambaye ni mmoja wa kaka zake Okebe, alisema huenda afisa huyo aligombana na mkewe ambaye alitoweka nyumba mnamo Februari mwaka, 2025.
Inasemekana kuwa mkewe Okebe alihamia eneo la Sori pamoja na wanawe lakini mumewe aliporejea kutoka kituo cha polisi cha Marsabit anakohudumu, aliamua kuwachukua watoto hao.
“Alimshawishi mkewe kwamba watoto hao wanapaswa kuendelea na masomo yao katika shule iliyoko karibu na kijiji cha Kagoga,” Bw Ochieng’ akasema.
Katika moja ya nyaraka zilizopatikana eneo la tukio, Okebe alisema kuwa alitarajiwa kurejea kazini Aprili 1 lakini hakurejea kwa sababu mmoja wa wakubwa wake anamhangaisha.
Nyaraka hizo ziliandikiwa mamake afisa huyo, mashemeji zake na wenzake kazini.
Okebe alieleza kuwa mambo yalikuwa yakimsumbua akilini mwake na asingevumilia na kutazama maisha yake yakiathirika.
Aliandika kuwa mmoja wa wakubwa wake alitishia kumwadhibu endapo asingerejea Marsabit kwa wakati.
“Hakutuongoza kwa usawa kwani kuna wenzetu ambao wangepewa mapumziko ya hadi miezi mitano. Lakini ilipotimu zamu yangu na mwenzangu (jina limebanwa) angeanza kututisha baada ya majuma matatu,” akaeleza.
Mnamo Jumapili jioni Kamishana wa Kaunti ya Homa Bay Lawrence Koilem aliongoza maafisa wa upelelezi kutoka vitengo mbalimbali katika eneo la tukio kuanza uchunguzi kuhusu tukio hilo.
“Tumempoteza afisa ambaye alikuwa anajua kazi yake. Matatizo ambayo yalichangia kifo chake ni mambo yanayoweza kusuluhishwa ikiwa watu wataongea,” Bw Koilel akaeleza.