Habari Mseto

Ibada ya wafu ya walioangamia ajalini kufanyika Jumatano

October 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON AMADALA

IBADA ya wafu ya watu 31 kutoka Kaunti ya Kakamega waliokufa kwenye ajali ya basi Kaunti ya Kericho itafanyika Jumatano.

Watu hao ni miongoni mwa 58 walioangamia, basi la Western Cross Sacco lilipohusika kwenye ajali Jumatano alfajiri.

Ratiba ya ibada hiyo iliyotayarishwa na serikali ya Kaunti inasema kwamba misa itafanyika katika uwanja wa Amalemba kuanzia saa tatu asubuhi.

Gavana Wycliffe Oparanya alisema serikali ya Kaunti italipa ada za mochari na kununua majeneza.

Jana, Bw Oparanya alishinda katika mkutano na maafisa wakuu wa serikali yake ambao walimweleza maandalizi yanavyoendelea.

Wengi wa waliokufa kwenye ajali hiyo walitoka Kaunti ya Kakamega.

Mipango imefanywa ya kuwa na magari ya kubeba maiti kusafirisha mili na mabasi ya kubeba jamaa na marafiki watakaohudhuria ibada hiyo. Dkt Dickson Muchana, ambaye ni mwanapatholojia katika hospitali ya Kaunti ya Kakamega alisema mipango ya kuchukua mili imekamilika.

Watu hao waliangamia eneo la Fort Ternan Kaunti ya Kericho na ilisemekana gari liliacha barabara na kubingiria. Watu 58 walipoteza maisha yao na 15 wakapata majeraha.

“Mili iko tayari kuchukuliwa kutoka mochari na familia na jamaa za marehemu,” alisema Dkt Muchana.

Mnamo Ijumaa, mahakama ya Molo iliagiza mmiliki wa basi hilo na meneja wake wazuiliwe kwa siku 10 ili polisi wakamilishe uchunguzi.

Hakimu Samuel Wahome alikubali ombi la mchunguzi kumzuilia Bw Cleophas Shimanyula na Bw Bernard Shitiabayi Ishindu.

Wawili hao waliokamatwa Jumatano wiki jana wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Londiani.