ICJ itatue zogo la umiliki wa Migingo – Orengo
NA ELISHA OTIENO
KIONGOZI wa Wachache katika Seneti James Orengo, sasa anaitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuingilia kati mzozo kuhusu umiliki wa kisiwa cha Migingo kati ya Kenya na Uganda.
Alisema kwamba, imechukua muda mrefu sana kwa mataifa hayo kusuluhusisha tofauti zao, hivyo hatua mbadala inahitajika kwa haraka.
“Namwomba Rais Uhuru Kenyatta na mkubwa wangu (Raila Odinga ) kuuwasilisha mzozo huu katika ICJ ili kuwaokoa wavuvi wetu dhidi ya kudhulumiwa kila mara na vikosi vya usalama vya Uganda katika Ziwa Viktoria,” akasema Bw Orengo, alipohutubu katika Kaunti ya Migori.
Bw Orengo, ambaye pia ni Seneta wa Siaya, alisema kuwa ramani zote za wakati wa ukoloni zinaoyesha kwamba, kisiwa hicho kiko katika himaya ya Kenya.
“Mzozo huu umezua usumbufu mwingi kwetu. Lazima tuusuluhishe kwa sasa, hasa wakati huu ambako kuna uthabiti wa kisiasa nchini,” akasema.
Alieleza kuwa mahakama hiyo imeshughulikia na kutatua mizozo kadhaa ya mipaka kati ya nchi mbalimbali.
Mdahalo uliibuliwa Bungeni majuzi na mbunge wa Nyatike, Tom Odege.
Mbunge huyo alisema kwamba Rais Kenyatta anapaswa kuangazia jawabu kwa mzozo huo, ikiwa angetaka kukumbukwa na Wakenya.
Alisema kuwa kufikia sasa, mzozo huo umedumu kwa zaidi ya miaka 15, akieleza imefika wakati ambapo unapaswa kusuluhishwa kabisa.
Akitoa hundi za basari katika eneobunge lake, Bw Odege alisema kuwa wavuvi na wafanyabiashara wa Kenya wangali wanahangaishwa na mamlaka za Uganda.
“Wavuvi wetu bado wanahangaishwa na vikosi vya usalana vya Uganda. Imefikia wakati ambapo lazima Rais Kenyatta na mwenzake, Yoweri Museveni walisuluhishe haraka,” akasema.
Wavuvi wanaohudumu katika kisiwa hicho, pia walisema kuwa wangali wanaendelea kutishwa na vikosi vya Uganda, bila usaidizi wowote kutoka kwa asasi za usalama za Kenya.
“Tunateseka sana mikononi mwa vikosi vya Uganda. Tunaomba suala hili lijumuishwe miongoni mwa yale yatakayoangaziwa katika mwafaka wa maelewano kati ya viongozi hao wawili,” akasema Bw Ken Oyoo, ambaye ni mvuvi.
Mwaka uliopita, Rais Kenyatta aliahidi kwamba angeanza harakati za kusuluhisha mzozo huo, ikiwa angechaguliwa kwa kipindi cha pili.