Habari Mseto

ICJ: Wakenya wa mapato madogo waangaziwe pia

March 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

TUME ya Mawakili na Majaji Nchini (ICJ) imetoa wito kwa serikali kuangazia maslahi ya wananchi wa mapato madogo wasiotegemea ajira wakati huu ambapo mikakati mingi imewekwa kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya corona nchini.

Kauli ya tume hiyo inatokana na hofu kwamba watu wanaotegemea vibarua kujikimu hawanufaiki kwa agizo la kufanyia kazi nyumbani, ICJ ikipendekeza serikali itangaze jinsi itakavyowasaidia kuendelea na maisha yao kama hapo awali.

Kupitia taarifa, mwenyekiti wa ICJ Kelvin Mogeni aliirai serikali kuchukua hatua ambazo zitahakikisha kwamba wananchi wanaotegemea vibarua hawahangaiki na kukosa chakula wakati huu mgumu.

“Kufanyia kazi nyumbani hakutakidhi mahitaji ya watu wasioajiriwa na serikali au kwenye kampuni za kibinafsi. Ikizingatiwa zaidi ya asilimia 83.6 ya Wakenya wapo kwenye kundi hili, inasikitisha kwamba hakuna chochote ambacho kimesemwa kuhakikisha hawateseki kupata mahitaji yao,” akasema Bw Omogeni.

Aidha tume hiyo ilipongeza serikali, Wizara ya Afya na serikali za kaunti kwa kutekeleza mikakati maridhawa kama njia ya kuzima maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Hata hivyo, walisema mikakati hiyo ni hutekelezwa tu mijini huku Wakenya wanaoishi mashambani na kwenye mitaa ya mabanda wakikosa kushirikishwa.

“Habari za tahadhari za kiafya kuhusu virusi vya corona hazijaenezwa mashinani na mitaa ya mabanda. Wakenya wanaoishi huku hufikiria hivi ni virusi vinavyoathiri watu wa mijini. Tunairai serikali ihakikishe wote wanajumuishwa katika vita vya kutokomeza corona,” akaongeza.

Mapendekezo mengine ya serikali iliyotolewa na tume hiyo ni usawazishaji wa bei ya bidhaa, dawa na vyakula na kupunguza ushuru unaotozwa kampuni au watu katika sekta za kibinafsi ambazo zimeathirika kiuchumi kutokana na virusi vya corona.

Aidha serikali za kaunti pia zimetakiwa kuondoa ada wanazotozwa wananchi kwa kutumia vyoo vya umma hadi kipindi hiki cha janga la corona kipite.

Wakati huo huo, chama cha Afya ya Umma kimelalamika kwamba juhudi za kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya corona nchini zinaendelea kutatizwa na ukosefu wa vifaa hitajika hospitalini.

Katibu Mkuu wa chama hicho Mohamed Buba alisema Ijumaa vifaa vinavyopatikana katika hospitali zilizoko kwenye kaunti ni vichache mno na iwapo janga hili litaenea zaidi, basi Kenya huenda ikajipata pabaya kuliko Italia au China zilizoripoti vifo vingi zaidi duniani kutokana na virusi vya corona.

Bw Buba alisisitiza kuwa serikali inafaa kuwashirikisha wahudumu wengi wa afya badala ya kuwatumia tu wale walioajiriwa au wanaohudumu kupitia kandarasi.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe wiki hii alitangaza kwamba watu saba wameambukizwa virusi vya corona nchini japo akasema wapo katika hali dhabiti wanapoendelea kutengwa hospitali za Mbagathi na Kenyatta.

“Virusi vya corona si mzaha na lazima serikali itekeleze juhudi zote muhimu kazuia maambukizi zaidi. Hata hivyo, hatuna vifaa vya kutosha hata katika kaunti zetu. Vilevile wahudumu wa afya hawatoshi iwapo idadi ya walioambukizwa itapanda zaidi,” akasema Bw Buba kwenye kikao na wanahabari.

“Vilevile mafunzo zaidi yanafaa kuandaliwa kwa wahudumu wetu ili wasiwe kwenye hatari ya kuambukizwa na kuhatarisha maisha yao. Hili ni suala ambalo linahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau wote kutoka sekta ya afya,” akaongeza.