• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
‘Idadi kubwa ya visa vya dhuluma za kimapenzi Nairobi inatisha’

‘Idadi kubwa ya visa vya dhuluma za kimapenzi Nairobi inatisha’

Na CAROLYNE AGOSA

VISA zaidi ya 4,000 vya dhuluma za kimapenzi viliripotiwa katika Kaunti ya Nairobi mwaka mmoja uliopita huku waathiriwa kadha wakiambukizwa virusi hatari vya HIV.

Aidha, msichana mmoja kati ya watatu nchini Kenya hudhulumiwa kimapenzi kabla kufikisha umri wa miaka 18.

Hayo yalifichuliwa katika hafla ya kuzindua programu ya simu (App) ya kupiga ripoti, kuhifadhi hati za waathiriwa kama vile ripoti ya daktari, na kufuatilia kesi za dhuluma kortini.

Afisa wa Kaunti ya Nairobi anayehusika na masuala ya dhuluma za kimapenzi Bi Roselyne Mkabana alisema kuwa jumla ya visa 4,517 viliripotiwa katika jiji kuu kati ya Julai 2018 na Juni 2019.

“Tulipokea ripoti za visa 4,517 vya dhuluma za kimapenzi jijini Nairobi. Kati yao kulikuwa na watoto 382 na walemavu 77. Aidha, waathiriwa 6 waliambukizwa virusi vya HIV kutokana na vitendo hivyo katili vya ubakaji,” alisema Bi Mkabana.

Aliongeza: “Hili ni tone tu la hesabu halisi inayoshuhudiwa mashinani kwani waathiriwa wengi bado wanahofu ya kupiga ripoti kwa sababu mbalimbali.”

Afisa huyo wa kaunti alikuwa akizungumza Jumatano katika hafla ya kuzindua programu ya simu (App) ya kupiga ripoti, kuhifadhi hati kama vile ripoti ya daktari na kufuatilia kesi

Programu hiyo kwa jina “SV_CaseStudy” imeundwa na wakfu wa kutetea waathiriwa wa dhuluma la Wangu Kanja Foundation kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu (UNFPA).

“Waathiriwa sasa wataweza kufikia hati zao kwa urahisi na kuondoa visa vya stakabadhi hizo kufichwa ama kupotea. Hii itapunguza mno muda wa kesi za dhuluma,” alieleza mwanzilishi wa wakfu huo, Bi Wangu Kanja.

Kwa sasa programu hiyo inatumika kwa simu za kisasa kupitia “Google Play” lakini wakfu huo ulisema kuwa unanuia kuzindua nambari ya ujumbe mfupi, short code, ili kutumiwa na wale wasio na simu za kisasa.

Watoto

Vilevile, Bi Kanja alisema kuwa wananuia kuimarisha programu hiyo ili watoto waathiriwa pia waweze kupiga ripoti za visa vyovyote vya dhuluma wanavyokumbana navyo.

Waziri Msaidizi wa Usalama wa Ndani Bw Patrick Ole Ntutu alipongeza programu hiyo akisema itachangia pakubwa kudhibiti visa vya dhuluma nchini.

“Itawafaa sana waathiriwa kwani hofu ya kujitokeza huwafanya kuumia kimya kimya. Programu hii itachangia pakubwa kuwapa haki na pia kukabiliana na wakosaji,” alisema alipotoa hotuba kwa niaba ya Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i.

  • Tags

You can share this post!

Jaji mkuu David Maraga afungua mahakama ya mjini Ruiru

Mfyatukaji stadi Moraa afuzu Riadha za Dunia

adminleo