Habari Mseto

IEBC iko sawa na makamishna watatu – Mahakama

August 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imekubalia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendelea kuhudumu ikiwa na makamishna watatu.

Jaji Wilfrida Okwany alisema idadi ya makamishna haiwezi kuwa kizingiti kwa tume hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake.

Jaji huyo alitupilia mbali kesi iliyokuwa inapinga IEBC kuendelea kutekeleza majukumu yake chini ya uongozi wa mwenyekiti wake Bw Wafula Chebukati.

Mahakama ilisema kuwako kwa nafasi katika tume hii hakupasi kuifanya mahakama “ kufutilia mbali huduma zake.”

Korti ilikuwa imeombwa itangaze kuwa IEBC haiwezi kutekeleza majukumu yake ikiwa na makamishna watatu.

IEBC ilikumbwa na hali ya suinto fahamu baada ya makamishna  Consolata Maina, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya kujiuzulu.

Wanne hao waling’atuka baada ya  kujiuzulu kwa kamishna mwingine Bi Roselyn Akobe.

Baada ya kuondoka kwa makamishna hao sasa IEBC imesalia na Bw Chebukati (mwenyekiti), Molu Boya na Profesa Abdi Guliye.

Mahakama ilikuwa imeombwa itangaze kuwa makamishna waliosalia hawawezi kuendeleza shughuli zake kama vile kusimamia chaguzi ndogo na masuala mengine ya tume.

Katika uamuzi wake Jaji Okwany alisema masuala ya uchaguzi husimamiwa na sheria zilizoko na “ kwamba sio makamishna wanaozitunga.”

Alisema hakuna chochote kinazuia tume kuendeleza chaguzi ndogo zinazotokana na kufutiliwa mbali kwa ushindi wa viongozi mbali mbali miongoni mwa Magavana, Wabunge na Wawakilishi katika serikali za mabunge.

“Suala la uchaguzi halitokani na maazimio yanayopitishwa na makamishna wa IEBC mbali ni masuala ya sheria,” alisema Jaji Okwany.

Alisema sio kamati za makamishna ya IEBC zinazoimbuka na miundo msingi ya kuendeleza uchaguzi mbali ni sheria zilizotungwa na kuidhinishwa na bunge.

Kile IEBC hufanya kupitia kwa wafanyakazi wake ni kuhakikisha sheria za uchaguzi zimefuatwa wakati wa zoezi la kuwateua wanaowania viti.

Jaji huyo alisema katiba imeweka utaratibu wa kuendeleza uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo.

“Chaguzi ndogo zitathibitiwa na sheria zilizopo za uchaguzi na wala sio mapendekezo ya wingi wa makamishna katika IEBC,” alisema Jaji Okwany.