Chebukati atoa ufafanuzi kumhusu Igathe
Na CHARLES WASONGA
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imefafanua habari kwamba ilitoa taarifa iliyoashiria kuwa inamtambua Bw Polycarp Igathe kwamba ndiye Naibu Gavana wa Nairobi.
Kwa mujibu wa habari zilizochapishwa katika magazeti ya humu nchini na kupeperushwa kwenye runinga mkurugenzi wa masuala ya sheria katika IEBC Michael Goa alinukuliwa akidai kuwa kufikia sasa tume hiyo haijapokea habari zozote kuhusu kujiuzulu kwa Igathe.
Bw Goa alikuwa akijibu barua ya Spika wa Bunge la Nairobi Beatrice Elachi ambaye alitaka ufafanuzi kuhusu pengo la uongozi katika Kaunti ya Nairobi.
“Kuhusiana na pengo la uongozi katika Kaunti ya Nairobi, kufikia sasa tume haijapokea barua yoyote rasmi kwamba Naibu Gavana alijiuzulu. Tunasikia habari hizo kupitia vyombo vya habari kama Wakenya wengine,” ikasema barua ya IEBC iliyowasilishwa mahakamani na Bw Goa.
Lakini mnamo Ijumaa, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alitoa taarifa akisema kuwa kampuni ya mawakili ya M/S Diro and Advocate iliiandikia barua ikitaka ushauri kuhusu hali ya Uongozi wa Serikali ya Kaunti ya Nairobi.
Ombi hilo liliwasilishwa kwa niaba ya Bunge la Kaunti ya Nairobi. Bunge hilo lilitaka kupata maelezo kuhusu hali ya serikali ya Nairobi baada ya Mahakama kumzuia Gavana Mike Sonko kuingia afisini mwake kutokana na kesi ya ufisadi inayomkabili.
“Lakini mnamo Januari 22, 2020, IEBC ilipokea barua nyingine kutoka kwa Gavana Mike Sonko kwamba amemteua Anne Mwenda kuwa Naibu Gavana, ishara kuwa kulikuwa na pengo katika afisi hiyo, kwa mujibu ya kipengee cha 180 (5) cha Katiba,” Bw Chebukati akasema.
Akaongeza: “Kwa hivyo, tume ingependa kufafanua kuwa haina mamlaka ya kisheria kuchapisha ilani ya kujiuzulu kwa afisa aliyechaguliwa. Wajibu wake ni kuchapisha katika gazeti rasmi la serikali jina la mshikilizi wa afisi ya kuchaguliwa.”
Kwa hivyo, Bw Chebukati anasema kuwa habari zinazoashiria kuwa Bw Igathe angali Naibu Gavana na kwamba kuna washikilizi wawili wa afisi hiyo ni za kupotosha na kuiharibia IEBC jina.
“IEBC inawashauri wadau kusaka thibitisho kutoka kwake kuhusu masuala nyeti kama haya badala ya kuzisambaza katika vyombo ya habari,” akasema.
Lakini maelezo ya Bw Goa yaliyotolewa Alhamisi mahakamani kwa niaba ya Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Hussein Marijan.