'Ikulu inatafuta makaa'
Na EDWIN OKOTH na PETER MBURU
IKULU Jumanne ilitangaza kuwa inatafuta mtu au mkandarasi wa kuiuzia makaa.
Kupitia tangazo katika magazeti, ilitoa tenda ya wazi kwa yeyote anayetaka, na aliye na uwezo wa kuiuzia gesi na makaa.
Ni hatua ambayo imewafanya watu wengi kushangaa kuwa hata Ikulu makaa hutumiwa, badala ya mbinu bora ambazo serikali imekuwa ikipendekeza kutumiwa na wananchi, na hatua ya kupigwa marufuku kwa ukataji miti.
Inadaiwa afisi ya Mkurugenzi wa Ikulu Kinuthia Mbugua ndiyo inasimamia masuala yote huko, japo hakupatikana kufafanua zaidi kuhusu tenda hiyo.
“Vijana, wanawake na walemavu watahitajika kuwasilisha vyeti vya usajili katika makundi hayo,” ilani ya tenda hiyo ikasema.
Lakini tangazo hilo limekosolewa na wengi, hasa kutokana na hali kuwa serikali ilipiga marufuku ukataji miti kuanzia 2018, ili kuwezesha nchi kuwa na wingi wa misitu kwa asilimia 10 ya sehemu yake ya nchi kavu.