• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
IMF, World Bank waapa kusaidia Kenya kuondoka orodha ya kitovu cha ‘pesa chafu’

IMF, World Bank waapa kusaidia Kenya kuondoka orodha ya kitovu cha ‘pesa chafu’

NA WANDERI KAMAU

MASHIRIKA ya Magharibi yameapa kuisaidia Kenya kuondoka kwenye orodha ya mataifa yanayoonekana kuwa kitovu cha ‘pesa chafu’ yaani ‘wash wash’.

Usaidizi huo ni kuhakikisha kwamba Kenya imezingatia Sheria na Kanuni za Kimataifa za Kukabiliana na  Ulanguzi wa Pesa, Ufadhili wa Ugaidi na Uenezaji wa Silaha za Maangamizi ya Halaiki.

Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung’u, aliiambia Kamati ya Kudhibiti Madeni na Ubinafsishaji ya Bunge la Kimataifa kwamba mashirika tofauti ya kifedha yameapa kuisaidia Kenya kuondoka kwenye orodha hiyo.

Hilo linafuatia uamuzi wa Jopo la Hatia za Kifedha (FATF) kuiweka Kenya kwenye orodha ya mataifa yasiyo na mikakati thabiti ya kukabiliana na uingizaji au uwepo wa ‘pesa chafu’ katika himaya yake.

Jopo hilo ndilo ndilo huendesha mikakati ya kukabiliana na uenezaji wa pesa chafu kote duniani.

Baadhi ya mashirika ambayo yameapa kuisaidia Kenya kutolewa kwenye orodha hiyo ni Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia, Uingereza na Amerika.

Ijumaa iliyopita, Kenya iliwekwa kwenye orodha ya mataifa 23 yanayofuatiliwa kwa karibu kwa kutokuwa na mikakati bora ya kudhibiti ueneaji wa pesa chafu katika himaya yake.

Kando na pesa chafu, mataifa hayo yamekuwa yakidaiwa kutoa mazingira ya ufadhili wa vitendo vya kigaidi.

Hatua ya Kenya kuwekwa kwenye orodha hiyo inamaanisha itakuwa ikifuatiliwa kwa ukaribu na jopo hilo, kuhakikisha imezingatia sheria za kimataifa zilizowekwa.

“Leo (Ijumaa) asubuhi, nilifanya mkutano na mashirika ya nje ambayo yamekuwa yakitukopesha pesa, ambapo yametuahidi kwamba nchi hii itaondolewa kwenye orodha hiyo. Tumeweka mikakati ya kisheria kuhakikisha kuwa tuna uwezo wa kukabiliana na uenezaji wa fedha hizo na vitendo vinavyohusiana na maovu hayo,” akasema Prof Ndung’u.

Waziri aliliambia Bunge kwamba hatua ya Kenya kuwekwa kwenye orodha hiyo haitaathiri uwezekano wake kupewa mikopo na mashirika ya kimataifa au uwekezaji.

“Hatupaswi kuwa na wasiwasi wowote kwani tuna uungwaji mkono kutoka kwa mashirika ya kifedha ya kimataifa,” akasema.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na hofu kwamba Kenya imekuwa ikitumiwa na baadhi ya watu wenye ushawishi kuendesha ulanguzi wa pesa.

  • Tags

You can share this post!

Magari ya umeme yanapunguza uharibifu wa mazingira na vifo,...

Hofu biashara zenye hatari ya milipuko zikitapakaa mitaani

T L