• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
IPSOS: Wakenya bado huchagua wanasiasa wakijua ni wafisadi

IPSOS: Wakenya bado huchagua wanasiasa wakijua ni wafisadi

Na PETER MBURU

MMOJA kati ya kila Wakenya kumi anaamini kuwa viongozi wafisadi bado wanaweza kuongoza vyema, utafiti umesema.

Utafiti huo wa kura ya maoni wa Ipsos aidha ulionyesha kuwa wafuasi wa chama cha Jubilee wana imani kubwa kidogo kuhusu kiongozi mfisadi kuongoza vyema wakilinganishwa na wale wa muungano wa Nasa.

Kulingana na matokeo ya kura hiyo ya maoni, asilimia 12 ya wafuasi wa Jubilee wanadhani kuwa kiongozi mfisadi anaweza kuongoza vyema, idadi ya juu ikilinganishwa na asilimia 7 ya wafuasi wa Nasa.

Hata hivyo, asilimia 87 ya wakenya kwa jumla, 86 ya wafuasi wa Jubilee na 90 ya wafuasi wa Nasa wanasema kuwa kiongozi mfisadi hawezi kuongoza vyema, ukasema utafiti huo.

Utafiti huo aidha ulionyesha kuwa asilimia 73 ya wakenya kwa jumla, 69 ya wafuasi wa Jubilee na 77 ya wafuasi wa Nasa hawaamini kuwa watu wanaohusishwa na visa vya ufisadi watahukumiwa.

Katika utafiti huo, wakenya wengi walishikilia dhana kuwa uwezekano wa mkenya wa kawaida kuhukumiwa na kuadhibiwa akifanya kosa kubwa uko juu, ikilinganishwa na watu maarufu.

“Ni asilimia 17 ya wakenya pekee waliosema kwa hakika kuwa watu maarufu wa kisiasa ama wa serikali ama wafanyabiashara wenye pesa watahukumiwa na kuadhibiwa wakifanya kosa kubwa, asilimia 22 wakisema inawezekana nao asilimia 58 wakisema haiwezekani kamwe,” akasema mtafiti mkuu wa Ipsos Prof Tom Wolf.

Hata hivyo, asilimia 77 ya wakenya walikiri kuwa mkenya wa kawaida akifanya kosa kubwa atahukumiwa na kuadhibiwa, asilimia 18 wakasema inawezekana huku asilimia 4 wakisema haiwezekani kwa mkenya wa kawaida kuhukumiwa na kufungwa akifanya kosa kubwa.

You can share this post!

IPSOS: Wafuasi wa Raila bado hawajamkubali Uhuru

Ajabu ya magari mengine ya serikali kuuzwa kwa Sh12,000

adminleo