Isiolo yazindua mpango wa miaka mitano kukabiliana na utapiamlo
Na WAWERU WAIRIMU
KAUNTI ya Isiolo imezindua mpango wa miaka mitano wa lishe bora katika jitihada za kupunguza utapiamlo ambao ni miongoni mwa hali zinazotatiza pakubwa maendeleo ya kaunti hiyo.
Utapiamlo, hasa miongoni mwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, linasalia kuwa tatizo kuu linalorejesha nyuma Kaunti ya Isiolo huku asilimia ya waathiriwa ikifikia 13.8 hadi 16.7 kwa mwaka.
Huku idadi kubwa ya wakazi wakishindwa kumudu lishe bora kwa sababu ya kiwango cha juu cha umaskini, Gavana Mohamed Kuti amepania kuhakikisha kwamba serikali yake inapunguza visa vya utapiamlo na kuimarisha viwango vya afya miongoni mwa wakazi.
Ili kukabiliana vilivyo na tatizo la lishe bora, serikali ya Kaunti ya Isiolo imeanzisha miradi ya kusimamia utoaji wa chakula kwa akina mama wajawazito na watoto, pamija na kuwawezesha maafisa wa afya kuwapa wakazi huduma za uhamasishaji kuhusu lishe.
Katika awamu ya kwanza ya mradi huo, Kaunti ya Isiolo tayari imeunda makundi 50 ya wanajamii watakaosimamiwa na maafisa wa afya wa kujitolea ili kufanikisha mpango wa kutolewa kwa huduma za afya na lishe bora katika maeneo ya mbali ndani ya kaunti.
Mbinu nyinginezo ambazo serikali ya Kaunti ya Isiolo imepania kushirikisha katika juhudi za kukabiliana na utapiamlo ni kutoa huduma za bure za afya na kimatibabu pamoja na chakula na dawa za kuwaongezea watoto hamu ya chakula ambayo itatolewa katika vituo vyote vya afya.
Miongoni mwa sababu zinazochangia utapiamlo katika Kaunti ya Isiolo ni umaskini unaochangia kutokuwepo kwa lishe bora na ugumu wa kumudu chakula miongoni mwa wakazi.
“Mbali na ufugaji, Gavana Kuti amehimiza wakazi wa Isiolo kukumbatia matumizi ya mbinu za kisasa za ukulima ili kuongeza kiwango cha chakula na upatikanaji wa lishe bora,” akasema Katibu wa Serikali ya Kaunti ya Isiolo, Ahmed Galgalo.
Kaunti ya Isiolo ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na ukame wa mara kwa mara na hivyo kusababisha viwango duni vya uzalishaji wa chakula, mazao ya ufugaji na ongezeko la magonjwa kutokana na hali duni ya usafi.
IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO