Itumbi na wengine wanne wapoteza kazi katika PSCU
Na CHARLES WASONGA
MKURUGENZI wa Mawasiliano ya Kidijitali Dennis Itumbi ni miongoni mwa maafisa watano wakuu katika kitengo cha mawasiliano ya Rais (PSCU) ambao wamefutwa kazi baada ya nyadhifa zao kufutiliwa mbali na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC).
Wengine waliopoteza kazi ni mkurugenzi wa mawasiliano katika kitengo cha uvumishaji James Kinyua, mkurugenzi wa kitengo cha uandishi wa hotuba Eric Ng’eno, Afisa Mkuu wa Habari John Ndolo na Mkurugenzi wa Tamasha na Uvumishaji katika asasi ya Urais David Nzioka.
Katika barua iliyotumwa kwa Katibu wa Utumishi wa Umma Mary Kimonye Afisa Mkuu wa PSC Simon Rotich alisema Jumatano nyadhifa hizo zimefutuliwa mbali katika jitihada za kupanga upya utendakazi serikalini.
“Kandarasi za watano hao zimesitishwa kulingana na vifungu vya utamatishaji katika kandarasi zao ili kutoa nafasi kwa wao kulipwa,” akasema Rotich.
Maafisa hao watano waliagizwa warejeshe mali yote ya serikali zikiwemo baji zao rasmi.
Baada ya kupokea habari kwamba amefutwa kazi, Bw Itumbi ambaye amekuwa akijitambulisha katika mtandao wa Twitter kama Mkurugenzi wa PSCU alifuta jina hilo na kujiita mfugaji wa nguruwe.
Miaka miwili iliyopita Bw Itumbi alihamishwa kutoka Ikulu hadi katika afisi ya Naibu Rais William Ruto jumba la Harambee Annex. Hata hivyo, alidumisha cheo chake cha mkurugenzi wa mawasiliano ya dijitali katika Ikulu.
Tangu wakati huo amekuwa mtetezi sugu wa Dkt Ruto huku akiwashambuliwa maafisa wakuu serikalini wakiwemo mawaziri, makatibu wa wizara na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti.
Mnamo Septemba mwaka jana Bw Itumbi alishtakiwa kwa tuhuma za kuandika barua feki yenye madai kuwa mawaziri fulani walipanga njama ya kumuua Naibu Rais.
Barua hiyo ilidai kwamba mawaziri hao watatu waliandaa mkutano katika mkahawa wa La Mada kando la barabara kuu ya Thika kujadili mikakati ya kutekeleza mauaji ya Dkt Ruto.
Mawaziri hao, Peter Munya (Kilimo), Sicily Kariuki (Maji) na Joe Mucheru (ICT), walikana madai hayo lakini baada ya kaundikisha taarifa katika makao makuu ya DCI.
Mnamo Novemba 27, 2019, Itumbi alifurushwa katika jukwaa la wageni waheshimiwa wakati wa uzinduzi rasmi wa ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.