Habari Mseto

'Iweje mhadhiri wa uuguzi hakuamini tiba ya hospitalini?'

October 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WAMBUI na CHARLES WASONGA

MWILI wa mwana wa kiume wa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi haungepatikana Alhamisi lau msomi huyo angelipa kodi ya nyumba ya Sh40,000 kwa wakati.

Mwili wa Emmanuel Solomon Inyama, 13, uliokuwa unaelekea kuoza ulipatikana sebuleni nyumbani kwao katika majengo ya makazi ya Kifaru, mtaa wa South B, Nairobi na msimamizi wa jengo hilo Bw Stephen Mwangi.

Mamake Bi Anna Hotannah Khahugan ni mhadhiri katika katika kitivo cha Uuguzi, Chuo Kikuu cha Nairobi.

Na baada ya mwili wa mtoto huyo kupatikana, mhadhiri huyo alipatikana akiwa amejificha jikoni na ndipo akakamatwa kama mshukiwa katika kifo hicho cha kutatanisha.

Bw Mwangi aliambia Taifa Leo kwamba alikuwa ameenda kuitisha kodi ya nyumba na ndipo akaona mwili sakafuni sebuleni.

“Nilibisha mlango na hakuna aliyejibu na ndipo nikaamua kumpigia simu. Ningesikia simu ikilia lakini hakuna aliyejibu. Niliingiwa na wasiwasi na nikaamua kuchungulia kupitia tundu fulani kwenye dirisha la sebuleni na ndipo nikaona mwili sakafuni ukiwa umefunikwa kwa blanketi,” akasema msimamizi huyo.

Akaongeza: “Nzi walikuwa wakiizunguka karibu ishara kuwa mwili huo ulikuwa umeanza kuoza.”

Bw Mwangi aliwajulisha polisi wa kituo cha Eneo la Viwandani ambao walivunja mlango, wakafunua mwili na kugundua ulikuwa wa Inyama.

Hadi kifo chake, Inyama alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba na alikuwa amejisajili kwa masomo ya ziada tangu Januari 2019.

Eneo la uhalifu

Polisi waliwaonya watu dhidi ya kuchungulia ndani ya nyumba hiyo kwa sababu ni eneo la uhalifu.

Majirani walisema mhadhiri huyo amekuwa akiishi katika jengo hilo kwa zaidi ya miaka mitano na alianza kudhihirisha tabia za kiajabu baada ya kujiunga na kanisa fulani.

“Alianza kuvalia mavazi marefu na kitambaa kichwani huku akiepuka kushiriki mazunguzo na watu. Mara kadha angejifungia nyumbani kwake kwa saa kadha na hakuzungumza na yeyote hata ndani ya lifti, akasema jirani ambaye aliomba kutotajwa jina.

Majirani walisema walimwona mvulana huyo mwisho mnamo Januari. Na licha ya mamake kubadili mienendo yake, walisema ufichuzi wa kifo cha mwanawe umewashtua zaidi.

Wapelelezi wanaochunguza kisa hicho wanasema mwanamke huyo alionekana kama mtu mwenye matatizo ya kiakili.

“Wakati mmoja aliambia polisi kwamba aligundua mwanawe amefariki siku tano zilizopita alipomgusa na kuhisi kuwa mwili umegeuka baridi. Alisema alichelea kuondoa mwili huo nyumbani kwake kwa imani kwamba angefufuka,” akasema mpelelezi.

Jengo hilo la makazi limewekwa kamera za CCTV, kulingana na msimamizi wake Bw Mwangi.

“Inashangaza kuwa aliweza kuishi kwa nyumba na mwili wa mwanawe ambao ulianza kuoza. Mwili huo utafanyia upasuaji kubaini chanzo cha kifo chake, “ akasema Afisa Mkuu wa Polisi, Nairobi Bw Philip Ndolo.