Jacque Maribe kizimbani kuhusu kesi ya mauaji inayomkabili mchumba wake
Na BENSON MATHEKA
MWANAHABARI wa televisheni ya Citizen, Jacque Maribe (pichani), alifikishwa katika mahakama ya Kiambu Jumatatu kuhusiana na mauaji ya Bi Monica Nyawira Kimani katika eneo la Kilimani, Nairobi.
Bi Maribe, ambaye husoma habari na pia ni ripota, alikamatwa Jumamosi usiku baada ya kuhojiwa mara kadhaa na polisi.
Mchumba wake Joseph Irungu Kuria ndiye mshukiwa mkuu kwenye mauaji hayo na anazuiliwa na polisi.
Polisi pia walifanya uchunguzi katika nyumba ya Bi Maribe iliyoko mtaa wa Royal Park, Langata, na kukagua gari lake ambalo Irungu alitumia usiku ambao Monica aliuawa.
Kisa hiki kimeongeza idadi ya wanahabari maarufu wa Kenya walioshtakiwa au kuhusishwa na mauaji.
Mnamo 2014, Bi Esther Arunga, aliyekuwa msomaji maarufu wa habari za runinga alishtakiwa nchini Australia kwa mauaji ya mtoto wake.
Bi Arunga alihusishwa na mauaji ya mtoto huyo ambayo mumewe Quincy Timberlake alikuwa mshukiwa mkuu.
Mnamo 2011, mwanahabari Moses Otieno Dola alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya mkewe Sarah Wambui Kabiru yaliyotokea nyumbani kwao mtaani Umoja jijini Nairobi.
Bi Kabiru, ambaye pia alikuwa mwanahabari wa runinga ya NTV alikufa katika hali ya kutatanisha mnamo Mei 1, 2011.
Bw Dola alikanusha mashtaka na kesi hiyo inaendelea katika Mahakama Kuu jijini Nairobi.
Mwanahabari mwingine aliyehusishwa na mauaji ni Louis Otieno, ambaye alikuwa msomaji maarufu wa habari za runinga.
Jina la Louis lilitajwa katika uchunguzi wa kifo cha Bi Careen Chepchumba Kili, ambaye mwili wake ulipatikana usiku wa Februari 14, 2012.
Sawa na Monica, Chepchumba alikuwa akiishi peke yake katika eneo la Kilimani, Nairobi.
Mwili wake ulipatikana kitandani na uchunguzi ulifichua kwamba alibakwa na kuuawa kwa kunyongwa.
Bw Otieno aliambia mahakama iliyochunguza mauaji ya Chepchumba kwamba hakumwua msichana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 26.
Hata hivyo, alikiri kwamba marehemu alikuwa rafiki yake mkubwa na kwamba hakuwa Nairobi siku ambayo aliuawa.
Faili ya polisi iliwasilishwa kortini baada ya polisi kusema hawakuweza kuhusisha yeyote na mauaji ya msichana huyo.
Kwenye uamuzi wa uchunguzi, mahakama ililaumu polisi kwa kuvuruga uchunguzi wa mauaji ya Bi Chepchumba hasa kwa kutochunguza simu za Bw Otieno kuthibitisha alikokuwa siku ambayo mauaji yalitokea.
Mahakama ilipendekeza polisi wachunguze upya mauaji ya msichana huyo ikiwa ni pamoja na kumfanyia Bw Otieno uchunguzi wa chembe chembe za damu (DNA).
Bw Otieno ali toa masharti kabla ya kukubali kufanyiwa uchunguzi mpya wa DNA.