Jacque Maribe afutiwa kosa la kumuua Monicah Kimani
NA HASSAN WANZALA
MTANGAZAJI Jacque Maribe atajutia kauli zake alipokuwa akijitetea katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani baada ya mahakama kutambua kwamba alifanya kosa la kudanganya afisa wa umma akijua anasema uongo.
Jaji Grace Nzioka akitoa hukumu mnamo Ijumaa alimpata na hatia mshtakiwa mkuu Joseph Irungu almaarufu Jowie ambaye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na mfanyabiashara huyo katika nyumba yake Lamuria Gardens usiku aliouawa mnamo Septemba 19, 2018.
Hata hivyo, jaji Nzioka alisema Bi Maribe alitoa ushahidi wa uongo kwa nia ya kumkinga Jowie dhidi ya shtaka la mauaji.
“Bi Maribe alitoa ushahidi wa uongo kwamba Jowie alipigwa risasi na majambazi nje ya nyumba yao katika mtaa wa Royal Park,” akasema Bi Nzioka.
Japo aliondolewa shtaka la mauaji, Bi Maribe huenda akafunguliwa mashtaka.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) inajua kazi yake ikitokea mshtakiwa anatoa ushahidi wa uongo.
Mamake mtangazaji huyo ameelezea furaha yake baada ya Bi Nzioka kutoa hukumu hiyo.
“Mimi ni mhubiri na ninachoweza kusema ni kwamba kila kitu hufanyika na sababu, tunawashukuru wote waliotembea nasi katika safari hii ngumu,” akasema mzazi huyo.
Wengine waliokuwa katika Mahakama ya Milimani kusimama na mtangazaji huyo ni babake, Bw Mwangi Maribe na bloga Dennis Itumbi ambaye ni rafiki yake wa muda mrefu.