Jadi Achode achaguliwa kinara wa Mahakama Kuu
Na BENSON MATHEKA
JAJI Lydia Achode Jumanne alichaguliwa jaji mpya msimamizi wa Mahakama Kuu kuchukua nafasi iliyoachwa na Jaji Richard Mwongo ambaye amehudumu kwa miaka mitano.
Kipindi cha Jaji Mwongo kilimalizika 2017.
Achode alichaguliwa na majaji wenzake katika uchaguzi uliosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mjini Mombasa.
Atakuwa jaji wa pili kushikilia wadhifa huo tangu katiba mpya ilipoanza kutumika 2010.
Kwenye uchaguzi huo, Jaji Achode alipata kura 43 kati ya 80 na kuwashinda majaji wenzake Mary Kasango na Asenath Ongeri.
Miongoni mwa majukumu yake yatakuwa ni kusimamia Mahakama Kuu na kuhakikisha kwamba shughuli zake hazitatiziki.
Atakuwa na mamlaka ya kuteua majaji wa kusikiliza kesi ikibidi kwa kushauriana na Jaji Mkuu au majukumu mengine atakayopatiwa na Jaji Mkuu.
Jaji Achode amepanda ngazi katika idara ya mahakama kutoka Hakimu katika mahakama ya Kericho mwaka wa 1986. Aliteuliwa jaji wa Mahakama Kuu 2011.
Amewahi kuhudumu kama msajili wa Mahakama Kuu.
Mnamo 2016, Jaji Achode aliteuliwa kuhudumu katika mahakama ya kusikiliza kesi za ufisadi na ni mwekahazina wa chama cha majaji wanawake nchini.