Jaji aagiza wakili wa Burundi akamatwe
Na RICHARD MUNGUTI
WAKILI wa taifa la Burundi amejipata taabani humu nchini kwa kukataa na stakabadhi za mahakama.
Jaji Maureen Onyango, aliamuru wakili huyo Cyprian Sabuku ashikwe na Polisi na kufikishwa mahakamani kueleza “ sababu asifungwe jela kwa kukatalia stakabadhi za kesi na agizo la korti.”
Bw Sabuku aliyeajiriwa na kampuni kubwa zaidi barani Afrika ya Bima almaarufu African Trade Insurance Agency (ATI) kama katibu aliagizwa atiwe baroni na Jaji Maureen Onyango wa mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi na waajiri (ELRC).
Shirika hilo la ATI limewashtakiwa na kinara wake Bw George Oduori Otieno akipinga agizo astaafishwe Julai mwaka huu.
Bw Otieno kupitia kwa wakili Titus Koceyo, ameshtaki ATI kwa kutangaza wadhifa anaohudumu kuwa wazi baada ya kufanyia marekebisho kandarasi ya ajira.
Katika marekebisho hayo, ATI imesema kuwa afisa mkuu wake atakuwa akihudumu kwa kipindi cha miaka mitano.
Awali ATI iliruhusu kinara wake ahudumu kwa vipindi vya miaka mitatu Bw Otieno aliajiriwa 2010 na amehudu sasa kwa miaka 10.
Katika kesi aliyoshtaki, Bw Otieno anasema anatakiwa kustaafu 2021 kwa vile ndiye anayehudumu kwa sasa na hajakamilisha kipindi chake.
Kwa mwezi mmoja mlalamishi hupokea mshahara wa Sh2.5m . Akijitetea Otieno anasema amekuba ATI hata Benki ya Dunia imekubali kuipa misaada ya kifedha.
Wakati Bw Koceyo alipeleka hati za kesi hiyo kwa Bw Sabuku alizitwaa na kukataa nazo akisema nchini kwa Burundian mmoja akikabidhiwa hati za kesi “ harudishi.”
Bw Sabuku alimtisha Bw Koceyo na afisa wa korti Bw Kennedy Oyoo. Jumatano Bw Koceyo alimshtaki Bw Sabuku kwa kukaidi sheria na utovu wa nidhamu.
Wakili huyo aliomba Bw Sabuku ashurutishwe kurudisha stakabadhi alizotwaa na kutiwa nguvuni na kushtakiwa kwa kukaidi agizo la korti.
Jaji Onyango alimwagiza afike kortini Alhamisi lakini akakataa kufika kortini ndipo polisi wakaagizwa wamkamate raia huyo wa kigeni.
Jaji Onyango alimwamuru Bw Sabuku amrudishie Bw Koceyo stakabadhi za kesi hiyo na kuamuru kesi isikizwe Mei 27, 2019.