Jaji Mkuu aamuru kesi ya magavana isikizwe wiki ijayo
Na RICHARD MUNGUTI na MERCY MWENDE
JAJI mkuu David Maraga ameshauri suluhu itafutwe haraka iwezekanavyo kwa lengo la kuepusha mitafaruku katika ufadhili wa serikali za kaunti.
Akiamuru walioshtakiwa na magavana 47 wawasilishe ushahidi katika mahakama ya juu kufikia Julai 22, 2019 saa kumi alasiri, Jaji Maraga alisema, “migongano na mitafaruku inaweza kuepukwa iwapo makubaliano kati ya pande zote itasakwa.”
Wakimjibu, magavana hao 47 walioshtaki asasi kadhaa za serikali walisema hawajakataa kusikizana kuhusu suala hili la mgawo na ufadhili wa kifedha kutoka kwa serikali kuu na wanachotaka ni suluhu ipatikane.
Mawakili Nzamba Kitonga, Fred Ngatia, Kamotho Waiganjo, Wangeci Thanje na S K Mwendwa walimweleza Jaji Maraga “tumejaribu tuwezavyo lakini tumegonga mwamba ndipo tumeamua kuwasilisha hii kesi kupata jibu.”
“Mapenzi yetu ni kupata suluhu haraka sio kuendelea na hii kesi. Misimamo mikali na baadhi ya asasi za serikali kuhusu ugavi wa pesa za kufanikisha maendeleo katika magatuzi ndio tatizo,” Bw Ngatia alisema.
Katika kesi hiyo, wanasema pesa zilizotengewa serikali za kaunti na serikali kuu zahitaji kuongezwa hadi Sh335 bilioni.
Bunge la kitaifa liliidhinisha serikali za kaunti zitengewe Sh316 bilioni kuendeleza shughuli zao.
Magavana wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza la magavana (CoG) Wyclife Oparanya wanadai kuwa Wizara ya Fedha na Bunge la Kitaifa zimefanya njama za kunyima serikali za kaunti pesa za kutosha kugharamia mahitaji.
Jaji Maraga aliamuru wahusika wote wawasilishe ushahidi ifikapo Jumatatu saa kumi na wafike kortini Julai 23 kupata mwelekeo.
Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi, amewasilisha ombi la kutaka kesi hiyo ya CoG itupiliwe mbali akisema haki za kila mmoja zilizingatiwa wakati wa kuandaliwa kwa makadirio ya matumizi ya pesa kutoka kwa hazina kuu.
Anasema kuwa kuna kesi nyingi zilizowasilishwa mahakamani kuhusu suala hili na zapasa kuamuliwa kwanza kabla ya mahakama kuu kutoa ushauri kuhusu suala hili la ugavi wa pesa.
Kushtaki
Alhamisi, Bunge la Seneti liliishtaki lile la kitaifa kuhusu sheria 24, ikiwemo hii ya ugavi wa pesa kwa serikali za kaunti.
Katika mahakama ya Nyeri, mfungwa aliyekuwa amefungwa kwa kipindi cha miaka kumi alitoroka katika jela moja mjini Nyeri alipokuwa anafanya zamu yake ya kila siku kama alivyokuwa ameagizwa na msimazi wake.
Geoffrey Macharia Gachigi alifungwa mnamo Oktoba 9, 2018, alipopatikana na makosa ya uhalifu katika eneo la Mukurwe-ini.
Afisa aliyekuwa akimsimamia gerezani aligundua kuwa mfungwa huyo hakuwa katika seli yake. Walifanya gwaride la wafungwa wote waliokuwepo, lakini hakuwepo.
Maafisa wa gereza walifahamisha vituo vya polisi mbalimbali kuhusu tukio hilo ili visaidie kumpata.
Alikamatwa Julai 17, 2019 katika jiji la Nairobi na kusindikizwa katika kituo cha polisi cha Nyeri ambapo alifunguliwa mashtaka ya kutoroka kutoka gerezani.
Alipofikishwa kortini jana, Gachigi alimweleza Hakimu mkuu mwandamizi, Bw Philip Mutua, kuwa alitoroka kutokana na mawazo mengi kuhusu familia.
“Nina mtoto aliye katika darasa la nane na anatarajia kufanya mtihani wa KCPE mwaka huu. Nilikuwa na mawazo mengi kumhusu nikahisi kuwa nilihitaji kuiona familia yangu,” akajieleza.
Hata hivyo, hakimu alimwongezea kifungo cha miaka mitatu ili asijaribu kurudia kitendo hicho tena.