• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
JAMHURI DEI: Juhudi kuleta usawa katika elimu zatiliwa mkazo

JAMHURI DEI: Juhudi kuleta usawa katika elimu zatiliwa mkazo

Na WANDERI KAMAU

BAADA ya Kenya kujinyakulia uhuru mnamo Desemba 12, 1963, mojawapo ya malengo makuu ya serikali ya Mzee Jomo Kenyatta yalikuwa ni kuimarisha kiwango cha elimu.

Miaka 56 baadaye, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imeanza utekelezaji wa mfumo mpya wa elimu wa 2-6-6-3, unaolenga kuwapa wanafunzi ujuzi wa taaluma mbalimbali kuanzia katika kiwango cha chini.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya elimu, mfumo wa 8-4-4 uliokuwepo awali umelaumiwa pakubwa kutilia maanani matokeo ya mitihani badala ya kuwapa wanafunzi mafunzo ambayo wanaweza kuyatumia kujiajiri wenyewe.

Mfumo huo ndio umelaumiwa kuchangia idadi kubwa ya vijana ambao hawana ajira nchini kufikia sasa.

Kulingana na Rais Kenyatta, mfumo wa 2-6-6-3 unalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata nafasi kuendeleza vipaji vyao katika mazingira ya wazi bila kuzingatia masuala ya mitihani.

“Huu ni mfumo tendaji unaolenga kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma kwa kisingizio cha kutopita mtihani wake,” akasema.

Chini ya mfumo huo, wanafunzi watasoma miaka miwili katika shule ya msingi (kiwango cha chini), miaka sita (kiwango cha juu katika shule ya msingi), miaka sita katika shule ya upili (kiwango cha chini na juu) na miaka mitatu katika chuo kikuu.

Tayari, majaribio ya mfumo huo yameanza kutekelezwa katika madarasa ya Pili na Tatu kote nchini.

Mnamo 1967, Kenya ilibuni mfumo wa elimu wa 7-4-2-3 sawa na Uganda na Tanzania, baada ya kubuniwa kwa Muungano wa Afrika Mashariki (EAC). Baada ya kusambaratika kwa EAC mnamo 1977, Kenya iliendeleza mfumo huo, lakini ikabadilisha majina ya mtihani wake.

Mtihani wa shule ya msingi uliitwa Cheti cha Shule ya Msingi (CPE) huku ule wa shule za upili ukiitwa Cheti cha Masomo Kenya (KCE). Mtihani wa shule ya upili katika kiwango cha juu uliitwa Mtihani wa Sekondari wa Ngazi ya Juu Kenya (KACE).

Hata hivyo, Rais Mstaafu Daniel Moi alibadilisha mfumo mnamo 1985 huo kuwa 8-4-4. Mfumo huo unatumika hadi sasa. Chini ya mfumo huo, mwanafunzi husoma miaka minane katika shule ya msingi, miaka minne katika shule ya upili na miaka minne katika chuo kikuu.

Mfumo huo umechangia sana katika ukuaji wa elimu, hasa idadi ya taasisi za elimu ya juu kama vyuo vikuu.

Mchango mkubwa wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki ulikuwa ni kuanzisha masomo ya shule ya msingi bila malipo mnamo 2003, hatua iliyoongeza idadi ya watoto wanaopokea elimu.

You can share this post!

JAMHURI DEI: Uhaba wa chakula bado donda ndugu mamia wakifa...

JAMHURI DEI: Wakenya bado walia kuhusu umiliki wa ardhi

adminleo