• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
JAMHURI DEI: Masuala ya ufisadi na usalama yatawala

JAMHURI DEI: Masuala ya ufisadi na usalama yatawala

Na WAANDISHI WETU

MAENEO tofauti ya nchi Jumanne yalijumuika na taifa kusherehekea maadhimisho ya miaka 55 tangu Kenya ilipopata uhuru, katika kaunti nyingi magavana na makamishna wa kaunti wakiongoza wananchi katika sherehe hizo.

Katika kanda pana ya pwani, suala la usalama lilipewa kipaumbele, haswa baada ya aliyekuwa naibu gavana wa kaunti ya Kilifi Kenneth Kamto kuuawa usiku wa kuamkia jana na majambazi wasiojulikana.

Viongozi pamoja na wakuu wa usalama kaunti za pwani walisisitiza umuhimu wa usalama, huku kukiitishwa ushirikiano baina ya wakazi, viongozi na asasi za usalama ili kuafikia utulivu.

Mamia ya wakazi wa kaunti ya kilifi walimiminika katika uwanja wa Karisa Maitha ambapo waliomboleza kifo cha Marehemu Kamto, bendera ya kaunti ikipeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya maombolezi. Katika kaunti ya Mombasa aidha hali ilikuwa sawia kwani kaunti hiyo imekumbwa na visa vya mauaji ya magenge siku za majuzi, Gavana Ali Joho akihimiza wakazi kujitolea kushiriki vita hivyo.

“Jumatatu tutaandaa mkutano na wakuu wa usalama kujadili suluhu kwa mambo haya kisha tuanzishe kampeni kwa jina ‘husika’ ili kila mmoja wetu awe sehemu ya kushiriki vita hivi vya utovu wa usalama,” akasema Gavana Joho.

Japo kamishna wa kaunti hiyo Evans Achoki aliwataka wazazi kuwarudi wanao, viongozi wengine walisema tatizo kuu ni ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana.

Hali ilikuwa sawia katika kaunti zingine za eneo hilo, kaunti ya Lamu kamishna wake Joseph Kanyiri akiongoza sherehe pamoja na naibu gavana Abdulhakim Aboud, Taita Taveta naibu gavana Majala Mlaghui pamoja na viongozi wengine, Kwale Gavana Salim Mvurya na katika kaunti ya Tana River.

Katika kaunti ya Machakos, vilio vya gavana Alfred Mutua kuwa kuna viongozi ambao wanampiga vita vilipatana na wito wa kamishna wa kaunti hiyo Abdillahi Galgalo kuwa akubali kushirikiana nao, baada ya viongozi wa kaunti hiyo kuamua kwa kauli moja kufanya kazi pamoja. Dkt Mutua hakuwa amehudhuria sherehe hizo, lakini ujumbe wake ulisomwa na mtu mwingine.

Katika kaunti ya Kisumu, Gavana Anyang’Nyongo alitumia fursa ya sherehe hizo kupiga marufuku uoshaji wa magari katika fuo za ziwa Victoria, akisema uchafu unaoingia majini unachafua ziwa hilo.

“Hakutakuwa na uoshaji wa magari katika ziwa hilo ama mto wowote kaunti hii ili tuweze kutunza maji, na hiyo ni amri ya serikali,” akasema Gavana Nyong’o.

Katika kaunti ya Kakamega, sherehe hizo ziliadhimishwa kwa nyimbo katika uwanja wa Bukhungu, japo mahudhurio yalikuwa ya chini. Gavana Wycliffe Oparanya na Kamishna wa Kaunti hiyo Abdirazak Jaldesa waliongoza maadhimisho, huku viongozi katika kaunti jirani ya Vihiga nao wakitumia fursa ya sherehe hizo kukashifu visa vya utovu wa usalama ambao umeshuhudiwa siku za majuzi.

Kaunti ya Kisii pia ilishuhudiwa kiwango cha chini cha watu waliohudhuria sherehe hizo, Gavana James Ongwae akiongoza waliohudhuria kusherehekea, na kutoa vitisho kwa wanaokula pesa za umma kuwa serikali yake haitawasaza.

Hali ilikuwa sawia katika kaunti ya Garissa ambayo pia idadi ndogo sana ya watu walijitokeza kwa maadhimisho ya sherehe hizo katika uwanja wa Bura Baraza, ambapo maafisa wa serikali ndio walionekana kuujaza.Kaunti zingine ambapo sherehe hizo ziliadhimishwa ni Kiambu (uwanja wa Thika), Tharaka Nithi (Shule ya upili ya Chuka Boys’), Uasin Gishu (64 Stadium), Laikipia, Homa Bay, Nakuru na Kitui.

You can share this post!

Joho, Waiguru, Haji, Kinoti na ‘Githeri Man’...

Raila sasa ataka mbunge wa Westlands kuwa gavana wa Nairobi...

adminleo