Habari Mseto

Jamii ya Wachangamwe yadai kupuuzwa na serikali

September 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA HAMISI NGOWA

Jamii ya Wachangamwe wanaoishi katika eneo bunge la Changamwe Kaunti ya Mombasa wameanzisha mikakati ya kuleta umoja miongoni mwao ili kutetea maslahi yao kwa pamoja.

Katika kile kinachoonekana kama mwamko mpya, wasomi kutoka jamii hiyo tayari wameanzisha vikao vya uhamasishaji ili kuwawezesha kutambua haki zao.

Miongoni mwa masuala muhimu yanayoangaziwa ni kuelimisha jamii hiyo kutambua haki zao za kimsingi katika Katiba ambazo wanadai serikali imezipuuza.

Kulingana na Mwenyekiti wa jamii hiyo, Bw Ahmed Mwidani, ni kwa kuitambua Katiba tu ambapo watu wa jamii hiyo wataweza kudai haki zao kutoka kwa serikali jinsi zilivyo katika Katiba.

Anasema ukosefu wa kutoijua Katiba, imetumiwa na serikali tangu jadi kuzidi kuikandamiza jamii hiyo kwa kuinyima haki zake za kimsingi ikiwemo ajira.

Kulingana naye, ni masikitiko makubwa kwamba miaka 52 tangu Kenya ilipojipatia uhuru, hakuna mtu wa kutoka katika jamii hiyo aliyewahi kuhudumu katika nyadhifa kubwa serikalini.

“Tuko na wasomi ambao wamebobea katika fani mbalimbali na wanaoweza kuhudumu katika idara mbalimbali za serikali na kuleta maendeleo, lakini cha kushangaza ni kwamba mtu wa jamii ya Wachangamwe hawajawahi kuteuliwa katika wadhifa wowote mkubwa serikalini,’’akasema.

Alisema kando na wasomi, vijana wa jamii hiyo pia wametengwa na serikali katika masuala ya uajiri akidai mashirika ya kiserikali yanayopatikana katika eneobunge hilo hayajatoa ajira kwa vijana wa jamii hiyo.

Alieleza kuwa kulingana na Katiba, mashirika ya serikali na vile vile ya kibinafsi, yanafaa kuwapa wenyeji kipaumbele katika masuala ya uajiri.

“Eneobunge la Changamwe ni miongoni mwa yale yanayochangia kwa asilimia kubwa ya uchumi wa serikali ya kitaifa na ile ya kaunti Mombasa kutokana na kuwepo kwa Bandari na idadi kubwa ya viwanda. Lakini ni masikitiko kwamba vijana wetu wanakaa bila ya kazi,’’ akatetea.

Sasa jamii hiyo inamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuitambua kwa kuiteua katika serikali yake kama anavyofanya kwa kuziteua jamii nyingine akisema imekuwa ikipigia kura upande wa serikali kwa lengo la kupata matunda japo matarajio yao husaulika pindi uchaguzi unapokamilika.

Akizungumza na Taifa Leo, Bw Mwidani aidha alisisitiza kwamba jamii hiyo itaendelea na vikao vya uhamasishaji hadi pale haki zao za kimsingi zitakapotekelezwa.

Alisema kikao cha kwanza tayari kiliandaliwa katika eneo la Jomvu ambako jamii hiyo iliweka mikakati kadhaa itakayohakikisha wanafikia malengo yao.