Habari Mseto

Jamii yaomba EACC ichunguze madai ya unyakuzi wa Msikiti 

Na JOSEPH WANGUI April 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAMII ya Waislamu imealika Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza madai ya unyakuzi wa msikiti wa kihistoria wa Kongo ulioko Diani, Kaunti ya Kwale, na mwekezaji wa kibinafsi aliyepata hatimiliki ya ardhi hiyo mnamo Februari.

Kulingana na wakili wa kundi hilo la Waislamu, Paul Mwangi, faili ya mahakama yenye kumbukumbu za kesi ambapo mchakato wa kupata hatimiliki hiyo ulianzia pia imepotea.

Awali, ardhi hiyo ilikuwa inamilikiwa na hayati Rais Daniel Arap Moi, ambaye alirudisha hatimiliki hiyo mwaka wa 2009 baada ya kugundua kuwa alikuwa amepewa kimakosa na Kamishna wa Ardhi wa zamani mnamo 1986.

Katika barua kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Abdi Mohammed, wakili Mwangi alisema kuwa ingawa msikiti huo wa kihistoria upo katika ardhi ya umma, hatimiliki hiyo ilipewa watu wawili binafsi mnamo Februari 17, 2025.

Wakili Mwangi anasema kuwa mwanzoni mwa mwaka huu, ardhi hiyo pia ilitangazwa kuuzwa kwa Sh1.4 bilioni na watu waliokabidhiwa umiliki wake mnamo 2005 kupitia kesi mahakamani.

Anaeleza kuwa msikiti huo ni mnara wa kihistoria uliohifadhiwa kisheria.

“Hukumu ya mahakama ilitolewa mwaka wa 2005. Tumekuwa tukijaribu kupitia faili hiyo katika Mahakama Kuu ya Mombasa ambapo amri hiyo ilitolewa lakini tunaambiwa kwamba faili ilipotea miaka michache iliyopita,” alisema wakili Mwangi katika barua ya kurasa saba iliyotumwa kwa EACC mnamo Jumanne, Aprili 1, 2025.

Barua hiyo inaonyesha kuwa hatimiliki hiyo imetolewa kwa watu wawili, lakini hatuwezi kuwataja kwa sababu za kisheria.

Aliongeza: “Ukweli na mazingira yote ya kesi hii yanaonyesha unyakuzi wa ardhi wa kawaida hapa Kenya, uliofanywa kwa mtindo wa kawaida, ukihusisha maafisa wakuu katika Wizara ya Ardhi, Mahakama Kuu ya Mombasa, na Tume ya Kitaifa ya Ardhi, katika mpango wa pamoja wa uhalifu wa kunyakua Msikiti wa Kongo na ardhi iliyo karibu.”

Wakili Mwangi anahoji kuwa ni jambo la kushangaza kwamba waliopata hatimiliki si wale waliokuwa wakipigania umiliki wa ardhi hiyo mahakamani.

Kesi hiyo ilikuwa kati ya Hassan Mohammed Hussein na Yusuf Kulmiye.

Aidha, anasisitiza kuwa hatimiliki hiyo ni batili kisheria na inakiuka Katiba kwa sababu ardhi hiyo haijawahi kuwa ya umma, na hata madai ya umiliki kwa kuishi kwa muda mrefu hayawezi kutumika.

Akisimulia historia ya ardhi hiyo, Bw Mwangi anasema kuwa mnamo 1986, ardhi hiyo ilipewa hayati Rais Moi kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, alipojua hilo mwaka wa 2009, aliirejesha na hatimiliki hiyo ikafutwa mara moja.

“Serikali kisha ikaiweka ardhi hiyo mikononi mwa jamii ya Waislamu wa Diani na kumteua Katibu wa Kudumu wa Hazina ya Kitaifa kuwa mdhamini wa Msikiti wa Kongo wa Kwale na Kituo cha Kiislamu cha Kwale ili kushikilia mali hiyo kwa manufaa yao,” anaeleza.

Anahoji kwa nini ilichukua miaka 19 (kutoka 2005 hadi 2025) ili hatimiliki ya ardhi hiyo ipatikane.

“Inashangaza kwamba hatimiliki hiyo inaonyesha kuwa ardhi hiyo inamilikiwa kwa mkataba wa miaka 99, ilhali umiliki wanaodai waliupata kutoka kwa Rais Moi mnamo 2005 ulikuwa wa kudumu,” alisema wakili Mwangi.

Msikiti wa Kongo ni wa zamani zaidi nchini Kenya na ulijengwa katika Karne ya 14. Umekuwa kituo cha Kiislamu kwa kipindi cha karne nyingi na unatambuliwa kama mnara wa kihistoria wa kitaifa.