• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Jela maisha kwa kuua shahidi katika kesi inayowakabili

Jela maisha kwa kuua shahidi katika kesi inayowakabili

Na JOSEPH WANGUI

WANAUME watatu walifungwa jela maisha kwa kumuua shahidi wa upande wa mashtaka aliyetoa ushahidi dhidi ya wawili hao katika kesi ya wizi wa mabavu miaka 16 iliyopita.

Daniel Karonji Wahome, David Gituku Kiruhi na Daniel Wachira Kiruhi walihukumiwa kufungwa jela maisha na Jaji Jairus Ngaah wa Mahakama Kuu ya Nyeri.

Jaji Ngaah alisema watatu hao hawakuonyesha majuto kwa kitendo chao na kwamba Wahome na Gituku awali walikuwa wamehukumiwa kunyongwa.

Watatu hao walimvamia na kumuua Bi Lucy Wangui Gitau mnamo Septemba 30, 2010. Wangui alikuwa jirani yao katika kijiji cha Gituiga, Othaya.

Wakati wa kitendo hicho, walikuwa na vifaa vilivyokuwa na makali ambavyo walitumia kumjeruhi Wangui kabla ya kuchoma nyumba yake. Alipata majeraha mabaya kwa kukatwa na kuchomeka sehemu kadhaa za mwili hali iliyosababisha kifo chake.

Upande wa Mashtaka ulifahamisha mahakama kwamba marehemu alikufa kifo cha uchungu na licha ya umri wake mkubwa, wavamizi hawakumhurumia.

Akitoa hukumu, Jaji Ngaah, alisema watatu hao walikuwa wakilipiza kisasi kwa sababu marehemu alikuwa amelalamika na kutoa ushahidi dhidi ya Bw Wahome na Bw Gituku katika kesi ya uhalifu waliyoshtakiwa katika mahakama ya hakimu.

Katika kesi hiyo Wahome na Gituku walishtakiwa kwa wizi wa mabavu ambapo walipatikana na hatia na kuhukumiwa kunyongwa.

Ilidaiwa kwamba walimnyang’anya Bi Wangui mali yake na kumjeruhi.

Baadaye walikata rufaa iliyofaulu na wakaachiliwa huru mnamo Agosti 5, 2010. Wiki nne baada ya kuachiliwa huru, walimshambulia Bi Wangui tena na kumuua.

Mahakama iliambiwa kwamba marehemu na mfanyakazi wake David Mwangi Maina walikuwa wamemaliza kula chakula cha jioni. Maina alipoondoka kuenda kulala katika nyumba yake iliyokuwa mita kumi kutoka jikoni, alisikia Wangui akipiga ukemi akijaribu kuita jina lake. Alitoka nje kuenda kumuokoa.

Alisema alipata marehemu akiwa amewasha moto akiendelea kushambuliwa na wanaume watatu ambao aliwatambua kwa kuwamulika kwa tochi yake na pia mwangaza wa moto huo.

Wahome na Gituku walikuwa majirani wa marehemu ambao alikuwa akiwafahamu na mara kwa mara walikuwa wakifungwa na kutoka jela.

Alisema alipoenda kumuokoa Wangui, wavamizi walimfukuza lakini akajifungia ndani ya nyumba yake na kuomba msaada.

Baada ya dakika ishirini alirudi jikoni na kumpata marehemu akiendelea kuchomeka kisha akazima moto akitumia maji.

Mwana wa marehemu John Macharia alisema aliposikia kilio cha mama yake, alitoka kuenda kumsaidia na akawaona washtakiwa wakikimbia.

Alisema aliwatambua kwa kuwamulika kwa tochi yake na pia kulikuwa na mbalamwezi.

  • Tags

You can share this post!

TSC kuwaajiri walimu 1,045

Kisura ajuta panya kutafuna maelfu aliyopora mumewe

adminleo