Jinsi maisha ya Mbarire yalivyogeuka baada ya kufichua makateli wa kahawa
NA WANDERI KAMAU
NAIBU Rais Rigathi Gachagua, Jumamosi alifichua jinsi maisha ya Gavana wa Embu Cecily Mbarire yalivyokuwa hatarini mara baada ya kuwataja hadharani makateli katika sekta ya kahawa.
Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha fedha katika Kaunti ya Murang’a, Bw Gachagua alifichua kwamba gavana huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alianza kufuatwa na magari yasiyo na nambari za usajili, siku chache baada ya kuzitaja kampuni alizoamini zilizokuwa zikiwapunja wakulima wa kahawa.
Bi Mbarire alizitaja kampuni hizo wakati wa Kongamano la Kahawa lililofanyika mjini Meru mnamo Juni 2023.
Bw Gachagua alisema kuwa serikali ililazimika kuimarisha usalama wa gavana huyo.
“Watu hao [makateli] walianza kumtafuta baada ya yeye kuwafichua. Nililazimika kuimarisha usalama wake. Walikuwa wakimfuata kwa magari kwa sababu alikuwa amewataja hadharani. Lazima tuwe na viongozi mashujaa,” akasema.
Alisema kuwa watu hao wana ushawishi mkubwa sana, hiyo ikiwa sababu kuu ambapo Rais William Ruto amempa jukumu la kuendesha mageuzi katika sekta ya kilimo, ni kutokana na tajriba yake pana katika masuala ya utawala na usalama.
“Watu hao wamekuwa wakiwapunja wakulima wetu. Hakuna mtu ambaye angetekeleza mageuzi hayo isipokuwa mimi na Rais Ruto. Hilo ndilo lilimfanya Rais kuniagiza kuendesha mageuzi hayo. Watu hao wana ushawishi sana. Huwa wanamhonga kila mtu isipokuwa Rais na Naibu wake. Pia, tuna usalama wa kutosha,” akaongeza.
Hata hivyo, aliongeza kuwa serikali itaendelea kutekeleza mageuzi hadi pale wakulima watakapofaidika kutokana na juhudi zao.
Kwenye kongamano hilo, Bi Mbarire alilalamika kuwa kampuni zenye nguvu na ushawishi mkubwa zilikuwa zikifaidika kwa kupata mamilioni ya pesa, huku wakulima wakiteseka.
Bi Mbarire alisema kuwa kampuni hizo ndizo zimekuwa zikidhibiti mauzo ya zao hilo katika nchi za nje.
“Sekta yetu ya kahawa inadhibitiwa na kampuni tatu. Huwa zinatumia ushawishi wake kuwapunja wakulima kwa kununua kahawa kutoka kwao kwa bei zinazotaka. Lazima mtindo huu ukome,” akasema Bi Mbarire.