Jinsi nauli ya juu SGR ilivyofukuza wasafiri
NA JOHN MUTUA
KUONGEZWA kwa nauli ya safari za garimoshi la kisasa (SGR) kati ya Nairobi na Mombasa mwanzoni mwa mwaka huu, kumesababisha abiria wengi kurejelea kupanda mabasi.
Ripoti ya mapato ya shirika la Reli nchini (Kenya Railways) inaonyesha kwamba idadi ya wasafiri ilipungua kwa abiria 65,833 kati ya Januari na Machi mwaka huu.
Ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka wa 2023, abiria walipungua kutoka 597,506 hadi 531,673. Mwisho wa mwaka jana, serikali ilitangaza kupandisha nauli za Madaraka Express kwa asilimia 50.
Ina maana kwamba abiria waliokuwa wakilipa Sh1,000 sasa wanalipa Sh1,500.
Wale wanaosafiri kwa behewa la watu mashuhuri sasa wanalipa Sh4,500 kutoka Sh3,000 hapo awali.
Ongezeko hilo la nauli lilipandisha mapato ya shirika la Kenya Railways hadi Sh880.8 milioni, ambalo ni ongezeko la asilimia 33 kutoka Sh660.2 milioni zilizopatikana katika kipindi sawa na hicho mwaka uliotangulia.
Hata hivyo, Madaraka Express bado haijajikwamua kutokana na mzigo mkubwa wa matumizi na gharama za usimamizi.
Hali hii inaifanya iendelee kutegemea pato la mlipa-ushuru kuendeleza shughuli zake, mbali na kulipa deni la mabilioni kwa benki ya China, iliyofadhili ujenzi ya reli hiyo ya kisasa kutoka Mombasa hadi Naivasha. Punde tu nauli za SGR zilipopandishwa, kulishuhudiwa kupungua kwa abiria mwezi Januari hadi 192,376 kutoka 247,011 waliotumia garimoshi hilo katika kipindi cha Januari ya mwaka 2023.
Kupanda kwa nauli hiyo kufikia Sh1,500 sasa kumewafanya baadhi ya wasafiri wasiokuwa na haraka ya kusafiri mchana, kurejelea mabasi na matatu zinazosafiri kati ya Nairobi na Mombasa.
Ingawa haijulikani hasa gharama ya kuendesha SGR ni kiasi gani, nyaraka zilizowasilishwa bungeni wakati mmoja zilionyesha kuwa kwa jumla kunahitajika Sh18 bilioni, kiwango kikubwa cha pesa kikiwa ni gharama ya kununua mafuta ya kuendesha mabogi hayo.
Wataalamu wa masuala ya uchumi wana wasiwasi kwamba zaidi ya miaka saba tangu SGR izinduliwe, serikali haijaanza kulipa mkopo wa Sh489.71 bilioni kwa Exim Bank ya China.