• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
‘Jogoo’ la Kanu lilipomeza ‘tinga’ la Raila

‘Jogoo’ la Kanu lilipomeza ‘tinga’ la Raila

Na JUSTUS OCHIENG

MAREHEMU Daniel Arap Moi atakumbukwa kama mwanasiasa ambaye alimpiga chenga Kiongozi wa ODM Raila Odinga kisiasa licha ya sifa zake nyota wa kusakata siasa.

Moi alifanikiwa kumshawishi Bw Odinga kwa kumuahidi kuwa angemuachia urais mnamo 2002 lakini ilipofika uchaguzi huo akamteua Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake.

Ilikuwa mnamo 2000 ambapo Mzee Moi alimshawishi Bw Odinga kuvunja chama chake cha LDP na kukiunganisha na Kanu

Bw Odinga alikuwa ameshiriki katika kinyang’anyiro cha urais mnamo 1997 na kuibuka katika nafasi ya tatu Moi akitangazwa mshindi.

Baada ya uchaguzi huo ambao ulikuwa wa mwisho kwa Moi, watu wa jamii ya Waluo walianza kujitenga na serikali.

Moi kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Nyanza Joseph Kaguthi, alitumia kanisa kurejesha uhusiano wake na eneo la Nyanza.

Uhusiano huo ulisababisha kubuniwa kwa Ushirikiano wa Makanisa ya Nyanza na Serikali ambapo mwenyekiti wake alikuwa Washington Ogonyo-Ngede na naibu wake alikuwa Askofu Julius Otieno.

“Ushirikiano huo uliwezesha watu wa Nyanza kufanya kazi na serikali na kunufaika kwa miradi ya maendeleo,” akasema Askofu Ngede.

“Tulimwendea Bw Odinga kumshawishi kufanya kazi na serikali na hapo ndipo alikubali kuunganisha chama chake cha NDP na Kanu,” anasema askofu Ngede wa Kanisa la Power of Jesus Around the World.

Ni baada ya muungano huo ambapo Waluo walianza kupewa nyadhifa serikalini, kulingana na Askofu Ngede.

“Tunafurahi kwa sababu muungano huo ulinusuru jamii ya Waluo dhidi ya kutupwa katika kaburi la sahau kisiasa,” anasema askofu.

Askofu Otieno anasema: “Rais Moi kwa kutumia busara yake alitualika nyumbani kwake Kabarak na kutuuliza jinsi tunavyoweza kushirikiana na serikali.” Alisema kuwa viongozi hao wa kidini ndio walitumika kama daraja kati ya Bw Odinga na Rais Moi.

“Moi alikuwa ametwambia kuwa Raila akikubali kushirikiana naye atamuachia urais 2002. Hii ilitusaidia kumshawishi Raila ndiposa akakubali kuvunja NDP na kujiunga na serikali,” akasimulia Askofu Otieno.

Baada ya kujiunga na Kanu, Bw Odinga aliteuliwa Katibu Mkuu na ndipo mtazamo kuwa jogoo la Kanu limemeza trakta ambayo ilikuwa alama ya NDP ukazuka.

Wadadisi wengine wanasema Bw Odinga alikubali kushirikiana na Kanu akiwa na nia ya kuharibu chama hicho kutoka ndani, jambo ambalo lilijitokeza miezi michache baadaye alipovunja muungano huo na kujiunga na ule wa Narc katika uchaguzi mkuu wa 2002 ambao Mwai Kibaki alishinda.

Moi alionekana kusaliti maelewano ya kumuachia Odinga madaraka kwa kumteua Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake na kwa hasira akaamua kumhujumu kwa kumuunga mkono Kibaki.

You can share this post!

Wanaume watatu waliomhangaisha Moi

Mzee Moi alikula kiamsha kinywa cha ugali kwa mboga...

adminleo