Habari MsetoSiasa

Joho na Kingi watofautiana kuhusu rais kutoka Pwani

March 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi wametofautiana kuhusiana na mpango wa kuwa na mwaniaji wa urais kutoka Pwani.

Huku Bw Joho akisisitiza kuwa yeye ndiye kiongozi anayefaa kupeperusha bendera ya kanda hiyo, Bw Kingi amesisitiza haja ya kuwepo umoja wa Pwani kabla ya uamuzi wa kuteuliwa kiongozi mwafaka.

Akizungumza katika hafla ya mchango wa elimu eneo la Mtomondoni kaunti ya Kilifi, Bw Kingi alisema kuwa haiwezekani wakati huu kusema kuwa Pwani itaongozwa na kiongozi fulani ilhali eneo hilo halijaungana pamoja.

“Kuna vitu ambavyo ni lazima tupambane navyo kabla ya kusema mtu fulani ndio atakayepeperusha bendera. Shida yetu ni umoja wa Pwani. Kwanza tunataka Pwani iwe kitu kimoja alafu ndio tuchague yule atakayetuwakilisha,” akasema Bw Kingi.

Bw Kingi alisema kuwa haiwezekani kwa viongozi wa Pwani kusema kuwa wapo na kiongozi ilhali kaunti hizo zimegawanyika.

“Mimi nitasemaje ndiye kiongozi wakati Kilifi inaelekea upande huu, Mombasa nayo inaelekea kule na Lamu, Tana River pamoja na Taita Taveta zinaelekea pande tofauti kisha mimi niseme naongoza Pwani. Itakuwa naongoza Pwani ama Kilifi,” akasema.

Bw Kingi alitamka hayo baada ya Gavana Joho kusisitiza kuwa atakuwepo kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2022 na kusema kuwa atamshinda asubuhi mapema mpinzani wake. ? “Kama wanadhani kuwa kiongozi wa Pwani hatokuwa kwenye debe basi watashangaa. Lazima wajipange kwa sababu kama ni kuanguka tutaanguka debeni,” Bw Joho aliuambia umati na kuongeza, “nyinyi mukiona jina la Joho ama Ruto mutampa nani kura?”

Mwaka 2017, Bw Joho na Bw Kingi walitangaza kuwa wataingia kwenye chemba na kufanya mazungumzo ya kukubaliana ni nani kati yao atakayepeperusha bendera ya Pwani.

Aidha, Jumapili Bw Kingi alisema kuwa kutekeleza mazungumzo baina yao ni jambo rahisi ila kazi ngumu ipo kwenye umoja wa Pwani.

“Sisi upande wetu kuzungumza ni jambo rahisi sana maana sisi ni marafiki lakini kazi ipo huo upande wenu. Ni lazima tuungane kama Wapwani na tusiwe wale watu wa kuabudu wengine wanapozungumza,” akasema Bw Kingi huku akitoa mifano ya viongozi wa zamani kutoka kanda hiyo ambao waliwahi kuwania kiti cha urais na kuangushwa na watu wa Pwani.

Wawili hao walizungumza baada ya baadhi ya viongozi waliokuwa kwenye mkutano huo kuregesha mwito wa wawili hao kuzungumza na kuchagua ni yupi atakayepeperusha bendera ya Pwani.

Maseneta na wabunge wa Pwani walisema kuwa kuna haja ya wawili hao kutangaza msimamo mapema ili kanda hiyo ijitayarishe mapema kwa siasa za mwaka 2022.

Viongozi hao pia walisisitiza haja ya umoja na kuongeza kuwa sifa za Bw Joho zinampa nafasi ya kuwepo kwenye siasa za kitaifa.

Viongozi hao walikuwa ni maseneta Stewart Madzayo, Mohammed Faki wa Mombasa na Issa Boy wa Kwale.

Wabunge walikuwa ni pamoja na Teddy Mwambire (Ganze), Ken Chonga (Kilifi South), William Kamoti (Rabai), Abdulswamad Nassir (Mvita), Omar Mwinyi (Changamwe) na Mwakilishi wa Kike Aisha Hussein.