'Jua Kali' watengewa kazi kwenye mpango wa ujenzi
Na VALENTINE OBARA
SERIKALI imetengea mafundi wa ‘Jua Kali’ kazi ya kutengeneza sehemu za nyumba kama vile milango na madirisha katika mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi alisema kuna Wakenya zaidi ya 175,000, ambao tayari wamejiandikisha katika mtandao wa ‘Nyumba Yangu’ kwa lengo la kununua nyumba hizo zitakazojengwa chini ya Ajenda Nne Kuu za maendeleo.
“Wakenya hawa watakuwa wa kwanza kutengewa nyumba zitakazojengwa. Zaidi ya hayo, mpango wa nyumba za bei nafuu unatarajiwa kutoa nafasi ya kustawisha sekta za humu nchini. Kwa msingi huu, tumeamua serikali itanunua vifaa kama vile milango na madirisha kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wa jua kali pekee,” akasema Rais kwenye hotuba yake kuhusu hali ya taifa jana bungeni.
Mbali na ujenzi wa nyumba za bei nafuu, ajenda nyingine kuu za Rais Kenyatta kabla aondoke mamlakani 2022 ni kuhusu uzalishaji wa chakula cha na sekta ya kiviwanda.
Kuhusu kilimo, Rais Kenyatta alikariri msimamo wa serikali kwamba wakulima wa kahawa wataanza kunufaika na Sh3 bilioni za malipo ya mapema kuanzia Julai, na ufufuzi wa viwanda 500 vya kahawa katika kaunti 31.
Alisema ripoti za jopokazi za kilimo cha miwa na mahindi zinatarajiwa baadaye mwezi huu, ili kutoa mwongozo kuhusu jinsi ya kutatua changamoto zinazokumba wakulima wa mazao hayo.
Katika sekta ya afya, alisema hatua zimepigwa vyema kuzindua mpango wa afya kwa wote katika kaunti za Isiolo, Machakos, Nyeri na Kisumu, na huduma hizo zitapelekwa kaunti zote katika kipindi cha fedha cha 2019/2020.
Rais alisifu hatua zilizopigwa kustawisha sekta ya viwanda.