Jumwa athubutu kusema atamwaibisha Raila katika uchaguzi mdogo
Na CHARLES LWANGA
MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa amefufua uadui wake na chama cha ODM baada ya kutangaza kuwa atatumia rasilimali zake zote kuhakikisha chama hicho hakipati kura yoyote katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa Ganda eneo la Malindi.
Bi Jumwa ambaye alitofautiana na chama viongozi wa ODM akiwemo Bw Raila Odinga baada ya kumpigia debe Naibu Rais William Ruto kumrithi Uhuru Kenyatta 2022, sasa anampigia debe mgombea wa kujitegemea, Bw Abdulrahaman Omar kuwania kiti hicho katika uchaguzi huo utakayofanywa Oktoba 17.
Bw Omar ambaye alijiuzulu kutoka ODM ili kugombea kama mgombeaji wa kujitegemea atakabiliana na Bw Reuben Katana wa ODM, Bw Joseph Kiponda (Jubilee Party) na Bw David Mutsanze wa Kadu Asili.
Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya Mahakama ya Rufaa kuidhinisha uamuzi wa Mahakama Kuu kufutilia mbali uchaguzi wa Bw Omar, ambaye alikuwa ametangazwa mshindi kupitia kwa tikiti ya ODM, na kuamuru kufanyika kwa uchaguzi upya.
Hii ni baada ya Bw Katana ambaye aliyegombea kwa chama cha Kadu Asili kuwasilisha ombi mahakamani kupinga uchaguzi huo mkuu wa Agosti 7 akidai haikufanywa kwa njia huru na haki.
Jumatatu iliyopita, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimwidhinisha Bw Katana kugombea kiti na baadaye kukutana na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho katika kaunti.
Kwa upande wake, Bi Jumwa alisema hatamuunga mkono mgombeaji wa ODM akisema chama hicho kilimchagua mgombeaji aliye kama ‘karatasi bure’ kwa sababu uamuzi huo haukuwa wa wakazi wa Ganda.
Akihutubia mamia ya watu alipozindua kampeni za kumpigia debe Bw Omar rasmi katika uwanja wa Kijiwetanga, Bi Jumwa alisema anampigia debe Bw Omar kwa sababu chama cha ODM hakikushauriana naye wakati kilichagua mgombeaji.
“Ikiwa ODM ingenishauri kuhusiana na mgombeaji, ningewambia Bw Omar ndiye anayefaa kugombea kiti hicho lakini walinipuuza na hawakujali kunishauri, kwa hivyo nitamuunga mkono Bw Omar asilimia 101,” alisema.
Mchujo
Pia, Bi Jumwa alishangaa kwa ni nini ODM ilitaka Bw Omar ashiriki kura ya mchujo badala ya kumpatia tiketi ya moja kwa moja baada ya Mahakama kufutilia mbali uchaguzi wake.
Isitoshe, alisema chama hicho kilikuwa kimemfurusha jinsi Bw Omar amefanywa lakini aliokolewa na mahakama na akataka ODM iheshimu uamuzi wa wakazi au sivyo watakiona cha mtema kuni katika uchaguzi wa Ganda.
“Tunaambia ODM kuwa makosa ambayo walifanya katika uchaguzi mdogo wa katika maeneo bunge ya Ugenya na Embakasi tayari wameyafanya hapa, sisi hatutatishwa wala kubabaishwa nao,” alisema.
Mbunge huyo alisema vita hivyo vya kisiasa si kati ya wagombeaji wa udiwani wa Ganda bali baina yake na chama cha ODM ili kupima ushupavu wao na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, ambaye pia ni naibu kinara wa ODM.
Bw Omar aliidhinshwa na IEBC jana kugombea kiti hicho baada ya kukusanya saini 500 kama inavyosatahili kikatiba.
Mbeleni, mgombeaji wa ODM ambaye aliandamana na madiwani wa ODM akiwemo Bw Nixon Mramba (Kakuyuni), Bw David Kadenge (Malindi Mjini), Bw Daniel Chiriba wa Jilore, waliahidi kupigia debe Bw Katana ili kurudisha ushindi huo kwa ODM.