Habari Mseto

Kabogo apanga kuwasilisha kesi mahakamani 'kukomboa wanunuaji wa vifurushi vya data'

May 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, William Kabogo, mtoto wa Mzee Gitau, sasa analenga ‘kukukomboa wateja wa Intaneti ya simu za rununu wawe huru na sio kwa kipimo, bali ni uwe huru kabisa.

Anasema kuwa atawasilisha kesi mahakamani kiwango sawa na vita vya ‘ukombozi dhidi ya ukoloni’, kupinga masharti ambayo kampuni za huduma za simu huwawekea wateja wanaponunua vifurushi vya data kwa Kiingereza ‘data bundles’.

Sio mara moja watumizi wa Intaneti hii ya simu wamenukuliwa wakiteta vikali, wakitisha kuhama kutoka kampuni hii hadi nyingine, wanapata hali ni sawa na wanarejea, yote yakiwa tisa, la kumi ikiwa kesi hii ya Kabogo iko na uwezekano wa kupata umaarufu miongoni mwa wateja hawa.

Kabogo anasema kuwa hajawahi kujitokeza madukani kujinunulia chumvi au sukari na mhudumu wa duka akampa masharti ya matumizi ya bidhaa hizo.

“Utahisi namna gani unapojitokeza dukani kununua mkate na muuzaji anakuambia ni lazima utumie mkate huo katika muda fulani la sivyo aje kukupokonya?” Kabogo anahoji.

Kabogo ambaye sio mara moja amenukuliwa hadharani akisema kuwa ana ukwasi tosha wa kushtaki na kujitetea mahakamani sasa amesema kuwa hizi kampuni hata ikiwa kila mwaka hutangaza faida ya mabilioni, atamenyana nazo kwa niaba ya wateja ili mteja anaporambaza kwa raha zake na kuzuru mitandao ya kijamii, awe yuko huru.

“Nataka mahakama iamuru kuwa ni kinyume cha sheria, ukiukaji maadili ya kibiashara na pia biashara huru kuwekewa vikwazo vya matumizi ya vifurushi vya data. Unaponunua data yako, inakuwa miliki yako uitumie kwa uwezo wako na kwa muda wako bila kuwekewa vikwazo kuwa uhalali wa ununuzi huo umedhibitiwa na muuzaji,” akasema.

Bw Kabogo amesema kuwa anaponunua data ya Sh1,000, hata akitaka kuiweka kama akiba ili aitumie miaka mitatu ijayo, “kwa kuwa nilinunua na ni yangu, matumizi yawe kwa raha zangu.”

Katika msingi huo, anasema kuwa uamuzi wa mahakama anaosaka ni kuwa, akishanunua data yake, ule ujumbe anaofaa kupata kutoka kwa kampuni iliyomuuzia ni kuwa “ahsante mteja wetu kwa kununua data ya Sh1,000 na ambayo sasa ni yako, uitumie na ikufae na tunakuenzi kama mteja wetu mpendwa. Ukishaitumia na iiishe kwa wakati wako, tutakuwa papa hapa kukuuzia tena.”

Hii ni kinyume na ambapo jumbe ambazo hufuata ununuzi huwa ni za kukuelezea kuhusu makataa ya matumizi ukipewa hadi mluda Fulani na masaa Fulani uwe umeitumia na ikaisha, la sivyo itwaliwe na uhitajike kununua data nyingine.