Kabogo: Uhuru alikuwa twiga, aliyeona mbali!
NA WANDERI KAMAU
ALIYEKUWA gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo, amesema kuwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alikuwa twiga aliyeona mbali kuhusu mambo ambayo baadaye yangewakumba wenyeji wa ukanda wa Mlima Kenya.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumatatu, Bw Kabogo alisema kuwa licha ya kufahamu hivyo, Bw Kenyatta aliamua kuwaambia wakazi kwa mbali, kwani wengi wao waliamua kumkaidi.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, Bw Kenyatta alimuunga mkono kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kuwania urais. Hata hivyo, eneo hilo lilimpigia kura kwa wingi Rais William Ruto.
“Bw Kenyatta aliamua kuachana nasi, kwani alijua hali ambayo ingekuwepo. Hata hivyo, aliamua kutupa tahadhari hizo akiwa mbali sana. Hilo ndilo limechangia hali ilivyo kiuchumi na kisiasa katika ukanda huu,” akasema Bw Kabogo.
Kwenye uchaguzi huo, Bw Kabogo aliwania ugavana kwa tiketi ya chama chake cha Tujibebe Wakenya Party (TWP), lakini akashindwa na gavana wa sasa, Kimani Wamatangi, aliyewania kwa tiketi ya chama tawala cha UDA.
Siku chache kabla ya uchaguzi huo, Bw Kabogo alijiunga na mrengo tawala wa Kenya Kwanza, lakini baadaye akatofautiana na uongozi wa muungano huo, katika kile alitaja “kubaguliwa kwa vyama vidogo vidogo.”
Tangu wakati huo, Bw Kabogo amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Ruto.
Kwenye mahojiano hayo, Bw Kabogo aliwalaumu viongozi ambao wamekuwa wakimlaumu Bw Kenyatta kwa changamoto zinazoikumba nchi, akisema wao ndio wako uongozini kwa sasa.
“Tunashinda tukiambiwa kuhusu vile Bw Kenyatta alifanya akiwa uongozini. Kwa sasa, hayuko uongozini. Yule aliye mamlakani ndiye anafaa kurekebisha matatizo yaliyopo,” akasema Bw Kabogo.
Kuhusu vita dhidi ya ufisadi nchini, Bw Kabogo alionya kwamba huenda maovu hayo yasiishe, ikiwa serikali haitababilisha mbinu na njia za kukabiliana nao.
“Lazima watu wanaotajwa kuhusika kwenye ufisadi wakabiliwe bila huruma na bila mapendeleo yoyote. Taasisi za kukabiliana na ufisadi lazima zifanye kazi yake kwa njia huru. Ikiwa hilo halitafanyika, ufisadi utabaki kuwa saratani isiyotibika,” akasema.