Habari Mseto

'Kadi za dijitali za HELB zitatumika kulipa karo na kodi ya nyumba'

August 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za mafunzo ambao hufadhiliwa na Bodi ya Masomo ya Juu (HELB) watahitajika kuwa na ‘smart card’.

Kadi hizo zitawasaidia kupokea ufadhili wao. Ripoti hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Elimu Bi Amina Mohamed Jumatano.

Wanafunzi watapokea mikopo yao kupitia kwa kadi hiyo kulipa karo na ada ya nyumba badala ya pesa hizo kuwekwa katika akaunti zao za benki.

Kadi hizo zitawezesha HELB kutuma mikopo kwa wakati ufaao na kuondoa makosa yaliyokuwa awali baada ya wanafunzi kutoa taarifa mbaya kuhusiana na nambari ya akaunti za benki.

Pia hatua hiyo inalenga kuimarisha uwazi huku kukiwa na ripoti za udanganyifu katika bodi hiyo.

“Kadi hizo zitahakikisha kuwa kuna usimamizi mwema wa fedha katika sekta ya elimu. Kadi hizo zitaanza kutumika Septemba mwaka huu,” alisema Bi Mohammed.

Vyuo vya mafunzo anuwai vitaanza kutekeleza matumizi ya kadi hiyo Desemba 31, alisema Bi Mohammed.