Kalonzo ageuka mtetezi sugu wa Uhuru mlimani
Na NDUNGU GACHANE
KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka amemtetea vikali Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya shutuma kwamba ametelekeza eneo la Mlima Kenya kimaendeleo.
Kulingana na Bw Musyoka, eneo hilo linaendelea kustawi kwa kasi inayohitajika.
Akizungumza katika Kanisa Katoliki la Mumbi wakati wa mazishi ya Bi Margaret Wangechi ambaye ni mamake Seneta Irungu Kangata mnamo Jumatatu, Musyoka alisema ametambua msimamo wa baadhi ya viongozi wa eneo hilo kwamba limetelekezwa kimaendeleo si wa kweli.
Bw Musyoka pia alitoa wito kwa Naibu Rais William Ruto ambaye pia alikuwepo katika mazishi hayo, apeane nafasi kwa asasi huru za serikali kuchunguza madai ya ufisadi.
“Nimesikia viongozi wakitaja miradi ikiwemo ile ya barabara na maji na baadhi yao imesemekana kutekelezwa na Naibu Rais. Lakini ni lazima tujue miradi hiyo haingefanikishwa bila kuidhinishwa na kiongozi wa taifa,” akaambia waombolezaji.
Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro alikuwa amedai barabara zilizoahidiwa na Bw Ruto ikiwemo ya Mukuria Hungu- Kayuyu- Gwa Thamnaki zimekaribia kukamilishwa huku ile ya Murang’a-Kiriani ambayo Naibu Rais aliahidi mwaka uliopita, iko karibu kuanzishwa.
Viongozi wengine wakiongozwa na Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria wamewahi kudai miradi ya maendeleo hupelekwa tu katika ngome za upinzani huku eneo ambalo lilimuunga Rais Kenyatta mkono kwa wingi likisahaulika.
Kuhusu ufisadi, kiongozi huyo wa Wiper alikashifu wanachama wa Jubilee kwa kuingiza siasa katika juhudi za kupambana na jinamizi hilo.